Kericho: Mwanafunzi wa chuo mwaka wa kwanza mwenye mimba ya miezi 9 ajinyonga

Sababu zilizomfanya mwanafunzi huyo wa miaka 19 ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi 9 kufa kwa kujiua hazikuweza kufahamika mara moja kwa vile barua ya kujiua haikupatikana kwake.

Muhtasari

• Mwanafunzi huyo alishukiwa kujinyonga jana usiku wakati kila mwanafamilia alikuwa amelala.

• Mwili wa marehemu uligunduliwa na mama wa marehemu ukining’inia juu ya paa.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Mshtuko na huzuni vilitanda katika eneo la Site and Service nje kidogo ya mji wa Kericho baada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo kikuu kujiua kwa sababu zisizoeleweka.

Kulingana na ripoti ya polisi, mwanafunzi huyo aliyetambulika kwa jina la Faith Charity Makhulu mwenye umri wa miaka 19 alifariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila iliyoning'inia juu ya paa kwenye korido ya nyumba yao ya makazi.

Sababu zilizomfanya mwanafunzi huyo ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi 9 kufa kwa kujiua hazikuweza kufahamika mara moja kwa vile barua ya kujiua haikupatikana kwake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa afisa mmoja wa utawala wa mkoa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mwanafunzi huyo alijinyonga baada ya mpenzi wake kudaiwa kumbwaga.

Mwili wa marehemu uligunduliwa na mama wa marehemu ukining’inia juu ya paa.

Mwanafunzi huyo alishukiwa kujinyonga jana usiku wakati kila mwanafamilia alikuwa amelala.

Mama huyo alitoa tahadhari iliyovuta hisia za majirani na wananchi wengine ambao walifika eneo la tukio na kujaribu kumuokoa marehemu lakini alikuwa ameshafariki dunia.

Kesi hiyo iliripotiwa baadaye katika Kituo cha Polisi cha Kericho ambapo maafisa wa polisi walikimbilia eneo la tukio, wakauondoa mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kericho.

Uchunguzi wa kisa hicho umeanzishwa ili kubaini chanzo cha tukio hilo.