Jumanne alasiri, naibu wa rais Rigathi Gachagua alimtembelea OCS wa polisi wa Juja aliyeripotiwa kushambuliwa kwa mshale na mgemaji wa pombe haramu huko Thika.
Gachagua alikuwa akizungumza baada ya kumtembelea OCS wa Kituo cha Polisi cha Juja, Inspekta Mkuu John Misoi, ambaye anapokea matibabu katika Hospitali ya Avenue mjini Thika kufuatia shambulio la watengenezaji pombe na wauzaji wa pombe haramu ya kuua watu huko Kiambu.
Aliandamana na Seneta wa Kiambu Karungo Thangwa na Mbunge wa Juja George Koimburi miongoni mwa viongozi wengine.
Naibu wa rais ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupambana dhidi ya uuzaji wa pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya alimwambia polisi huyo kwamba alimtembelea ili kumpa moyo.
“Tunakutakia mema, hii ni kadi kwako kuhisi nafuu, utakuwa sawa, ujue kwamba tunakuthamini, unajua mageuzi ambayo tunazidi kusukuma kuhusu bima ya afya kwa maafisa wa polisi ambao wanajeruhiwa wakiwa katika majukumu yao na mambo mengine yote tunayofanya kuhakikisha huduma ya polisi inakuwa afadhali,” Gachagua alisema.