Kitengela: Baba amuua bintiye kisha kujiua mwenyewe baada ya mkewe kutoroka ndoa

Mzee huyo alisemekana kuacha barua iliyotoa sababu za kutekeleza maafa hayo, akisema kuwa alitaka kumpa funzo mkewe kwa kumpotezea muda mwingi kwenye ndoa kisha kumtoroka.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa majirani ambao walizungumza na toleo la Naton.africa, walisikia vilio na nduru za kuomba msaada kutoka kwa nyumba hiyo

Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Image: Maktaba//The Star

Hali ya majonzi na simanzi viligubika mji wa Kitengela katika kaunti ya Kajiado baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 58 kumuua bintiye kinyama kisha kujiua mwenyewe katika kile kilichotajwa kuwa ni mzozo wa mapenzi kweney ndoa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, kisa hicho cha kushangaza kilijiri alasiri ya Jumapili.

Baba huyo alimuua bintiye wa miaka 16, ambaye alikuwa amekuja kumtembelea akitokea kwa mama yake ambaye walitengana na babake mizi michache iliyopita kutokana na mzozo wa ugomvi katika ndoa yao.

Kwa mujibu wa majirani ambao walizungumza na toleo la Naton.africa, walisikia vilio na nduru za kuomba msaada kutoka kwa nyumba hiyo

Walisema walisikia vurugu ambazo hazikuendelea kwa muda mrefu kabla ya kimya kutanda na baadae wakabaini kwamba baba huyo amemuua binti yake na kujiua mwenyewe pia.

“Tulisikia kelele ambazo hazikudumu kwa muda kisha kimya kikatanda, inasikitisha sana kwamba hatukuweza kumsaidia binti yule,” mmoja wa majirani alinukuliwa na jarida hilo.

Polisi walifika na kuchukua miili hiyo huku uchunguzi ukianzishwa.

 Walisema kwamba mwili wa binti ulipatikana na majeraha ya visu kwenye mgongo na kifuani huku babake pia akipatikana na majeraha ya visu kwenye kwenye tumbo.

Mzee huyo alisemekana kuacha barua iliyotoa sababu za kutekeleza maafa hayo, akisema kuwa alitaka kumpa funzo mkewe.

“Nilikuambia ya kwamba unacheza na mtu ambaye hujui unaniona tu, sasa hiyo ndio faida ulitaka kutoka kwangu, mimi ni yule ulidharau. Mimi naenda kupumzika, baki na kidonda cha maisha, hiyo ndio faida kwangu kwa miaka uliyonipotezea,” sehemu ya barua hiyo ilinukuliwa na Nation.africa.