Mpango wa kuanzisha ushuru mpya wazua hasira Kenya

Serikali ya Kenya inapanga kuanzisha ushuru mpya na ulioimarishwa katika sheria ya hivi punde.

Muhtasari

•Bei ya mkate inatarajiwa kuongezeka baada ya hazina ya kitaifa kupendekeza kuondoa bidhaa kuu kuu kutoka kwa orodha ya bidhaa zisizokatwa ushuru.

•Upinzani umetishia kufanya maandamano kote nchini ikiwa serikali itaendelea na hatua mpya za ushuru.

Image: BBC

Serikali ya Kenya inapanga kuanzisha ushuru mpya na ulioimarishwa katika sheria ya hivi punde inayopendekezwa ambayo imezua ukosoaji mkubwa nchini.

Bei ya mkate inatarajiwa kuongezeka baada ya hazina ya kitaifa kupendekeza kuondoa bidhaa kuu kuu kutoka kwa orodha ya bidhaa zisizokatwa ushuru, orodha ya msamaha wa ushuru wa ziada (VAT)

Gharama ya kutuma pesa kwa simu, muda wa maongezi na data pia inatazamiwa kupanda huku serikali ikipanga kuongeza ushuru wa ziada wa dola bilioni 2.4 za Kimarekani katika mwaka wa fedha unaoanza Julai.

Katika mapendekezo yaliyotolewa katika Mswada wa Fedha wa 2024 uliochapishwa Jumamosi, serikali pia inapanga kuanzisha ushuru mpya wa magari ambao utawafanya wenye magari kulipa hadi dola 750 kila mwaka ili kuendesha magari yao.

Ushuru huo mpya ni sehemu ya msururu wa hatua za kifedha zilizoanzishwa na serikali ya Rais William Ruto kufadhili miradi yake mikubwa ya miundombinu na kijamii.

Hatua hiyo imezua ukosoaji mkali huku wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu wakiitaja kuwa "mzigo".

Upinzani umetishia kufanya maandamano kote nchini ikiwa serikali itaendelea na hatua mpya za ushuru.

Mwaka jana, serikali ilianzisha aina kadhaa za ushuru, ikiwa ni pamoja na ushuru wa nyumba uliozua utata, licha ya pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya Wakenya.