Waathiriwa wa Mafuriko wahamishwe hadi kwenye nyumba za bei nafuu, Karua asema

Kuwapa nyumba za muda na kuwahamishia kwenye nyumba za bei nafuu ambazo zimejengwa kwa ushuru wetu

Muhtasari

•Waathiriwa wa Mafuriko Wahamishwe hadi kwenye Nyumba za bei nafuu.

•Maisha ni magumu kwa sababu ya gharama ya maisha, kuna wanawake ambao hawana cha kuwapa watoto wao wengine wameteseka kutokana na mafuriko.

Image: Martha Karua// Twitter

Kiongozi wa Chama cha Narc Kenya Martha Karua ameiomba serikali kuwapa makazi waathiriwa wa mafuriko katika nyumba zilizojengwa chini ya mpango wa nyumba za bei nafuu.

Kulingana na Karua, serikali inabeba jukumu la kusuluhisha familia zilizoathiriwa na kutoa mahitaji yao ya kimsingi.

“Maisha ni magumu kwa sababu ya gharama ya maisha, kuna wanawake ambao hawana cha kuwapa watoto wao wengine wameteseka kutokana na mafuriko…. Watoto wao wamekufa na wameachwa bila makao. Kodi zetu zinapaswa kukidhi mahitaji yao. Inatosha kutunza mahitaji yao ya elimu, matibabu na makazi. Kuwapa nyumba za muda na kuwahamishia kwenye nyumba za bei nafuu ambazo zimejengwa kwa ushuru wetu,” Karua alisema.

Pia alikashifu serikali ya Kenya Kwanza kwa pendekezo la Mswada wa Fedha wa 2024.

Karua alisema kuwa kadri katiba inavyoruhusu utozaji ushuru, mapendekezo ya ushuru katika Mswada wa Fedha ni sawa na yale yaliyowekwa wakati wa ukoloni.

“Ushuru lazima ulipwe, lakini huwezi kutoza (Wakenya) hadi unyime chakula duni. Huwezi kutoza ushuru hadi mtoto wa maskini alale njaa na kushindwa kwenda shule,” alisema.

Muungano wa Azimio la Umoja umekemea Kenya Kwanza kwa mapendekezo ya ushuru, na kutishia kurejeshwa kwa maandamano ya nchi nzima iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa.

"Hatuwezi kuruhusu ushuru huu wa adhabu ambao unawasonga Wakenya," Kalonzo Musyoka alisema Jumapili.

Kwa upande wake, Eugene Wamalwa alishutumu serikali kwa kuwapuuza Wakenya ambao hawana uwezo wa kumudu mlo kutokana na gharama ya juu ya maisha.

"Serikali ya Kenya Kwanza haina fununu kuhusu kile ambacho Wakenya wanapitia katika nyakati hizi ngumu kiuchumi," alisema Wamalwa.