Ni wakati wa kuacha kutoza ushuru kwa mapato-Kioni kwa Ruto

Kioni alisema ni muhimu kuwa na uwiano katika utozaji ushuru ili kutowalemea Wakenya.

Muhtasari
  • Akizungumza siku ya Alhamisi wakati wa mahojiano kwenye TV47, Kioni alisema mapato ya ziada ya ushuru yanawafanya Wakenya kuwa maskini zaidi kuliko walivyo.
JEREMIAH KIONI
Image: ENOS TECHE

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ametoa maoni kuwa ni wakati wa Rais William Ruto kutoza ushuru na sio mapato.

Akizungumza siku ya Alhamisi wakati wa mahojiano kwenye TV47, Kioni alisema mapato ya ziada ya ushuru yanawafanya Wakenya kuwa maskini zaidi kuliko walivyo.

"Huu ni wakati wa kuachana na kutoza ushuru kwa mapato. Hata kama tuna matatizo kama nchi, huwezi kamwe kuwatoza watu wako ushuru kiasi kwamba wanaweza kuwa maskini," Kioni alisema.

"Kama Wakenya, lazima tuanze kujiuliza, nini maana ya kulipa ushuru?" Kioni alisema.

Alisema biashara kote nchini kwa sasa zinakwama kutokana na ushuru mkubwa unaosababisha ugumu wa kuendesha shughuli zao za kila siku.

Kioni alisema ni muhimu kuwa na uwiano katika utozaji ushuru ili kutowalemea Wakenya.

"Sawazisha bajeti yako. Sawazisha uwezo wako wa kuongeza mapato na uwezo wako wa kutumia. Hii ni kanuni ambayo lazima itekelezwe kote nchini," Kioni alisema.

Haya yanajiri baada ya Rais Ruto kusema ananuia kuongeza kiwango cha wastani cha ushuru nchini kutoka asilimia 14 hadi 16 kufikia mwisho wa 2024 na analenga kati ya asilimia 20 na 22 kufikia mwisho wa muhula wake wa uongozi.

"Dhamira yangu ni kusukuma Kenya, mwaka huu tutakuwa asilimia 16. Nataka katika muhula wangu, Mungu akipenda, niiachie kati ya asilimia 20 na 22," Ruto alisema.

"Itakuwa ngumu, nina mambo mengi ya kufanya, watu watalalamika lakini najua watashukuru. Inabidi tuanze kuishi kulingana na uwezo wetu."

Ruto alitetea mpango wa serikali wa kutoza ushuru wa ziada kwa Wakenya, akisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuiondoa nchi katika madeni.

"Sitasimamia nchi iliyofilisika, sitasimamia nchi ambayo ina madeni. Tunapaswa kupunguza matumizi yetu," Ruto alisema.

Alizungumza Jumanne wakati wa makubaliano na wanafunzi wa Shule ya Biashara ya Havard kuhusu uwezo wa kibiashara na uwekezaji barani Afrika.