Tazama maeneo yatakayoathirika na kukatizwa kwa umeme leo, Jumapili- KPLC

KPLC imesema baadhi ya maeneo ya kaunti tano za Kenya yatakosa umeme mchana wa Jumapili.

Muhtasari

•Kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanyiwa kwenye mitambo.

•Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Nairobi, Uasin Gishu, Kisii, Mombasa na Kilifi.

Kenya Power
Image: HISANI

KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumapili, Mei 26.

Katika taarifa ya Jumamosi jioni, kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanyiwa kwenye mitambo.

Walisema baadhi ya maeneo ya kaunti tano za Kenya yatakosa umeme kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na moja jioni.Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Nairobi, Uasin Gishu, Kisii, Mombasa na Kilifi.

Katika kaunti ya Nairobi, sehemu kadhaa za mtaa wa Westlands zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja.

Kituo cha Sinendet katika kaunti ya Uasin Gishu kitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa nne asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Baadhi ya sehemu za mji wa Kisii katika kaunti ya Kisii zitakosa umeme kati ya saa moja na dakika ishirini asubuhi na saa kumi na dakika ishirini alasiri.

Sehemu kadhaa za maeneo ya Ganjoni na Kizingo katika kaunti ya Mombasa zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Wakati huohuo, baadhi ya sehemu za maeneo ya Mtwapa na Kanamai katika kaunti ya Kilifi pia zitashuhudia kukatizwa kwa umeme.