Wazalishaji bidhaa watishia kuhamia Tanzania iwapo mswada wa fedha 2024 utapitishwa jinsi ulivyo

Kamati ya fedha ya mipango ya kitaifa inapendekeza katika mswada wa fedha 2024 kuwekwa kwa ushuru wa 25% katika bidhaa za mafuta ya kula, hatua ambayo itapelekea bei ya bidhaa hiyo kuongezeka mara dufu.

Muhtasari

 
• Wadau wengine waliojitokeza kutoa maoni yao mbele ya kamati ya bunge inayoshughulikia mswada huo wa fedha waliteta kwamba mchakato wa kutoa maoni huishia tu kuwa pambe

Chama cha wazalishaji wa bidhaa mbalimbali humu nchini kimetishia kufunga makampuni yao na kuhamishia biashara zao katika taifa jirani la Tanzania iwapo mswada wa fedha wa 2024 utapitishwa bila kufanyiwa marekebisho.

Waliyasema haya wakati wa kutoa mapendekezo na maoni yao kuhusu mswada huo wa fedha ambapo walisema kwamba ushuru unaopendekezwa katika mswada huo unanuia kukandamiza biashara zao.

Walisema kwamba biashara yoyote lengo ni kutengeneza faida, lakini ikiwa mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, ina maana kwamba watakuwa wanahesabu hasara na si faida, jambo ambalo litawafanya baadhi yao kusitisha huduma zao za utengenezaji bidhaa humu nchini na kuhamia Tanzania.

“Ikiwa tutaendelea katika mkondo huu, huenda tutafunga biashara zetu na kuelekea Tanzania ambapo wawekezaji wanavutiwa. Kama mmoja alivyosema awali, biashara ni kuhusu kutengeneza faida, kama hautatengeneza pesa Kenya, unaenda na kutengeneza pesa Tanzania na Kenya litabaki kuwa taifa la kufanya biashara nao,” mmoja alisema.

 Wadau wengine waliojitokeza kutoa maoni yao mbele ya kamati ya bunge inayoshughulikia mswada huo wa fedha waliteta kwamba mchakato wa kutoa maoni huishia tu kuwa pambe na wala maoni ya kuwasitiri wananchi aghalabu huwa yanapuuziliwa mbali.

Baadhi ya mapendekezo katika mswada huo wa fedha 2024 yanalenga kuwaathiri moja kwa moja wanancho wa kawaida kwa kuongezwa kwa ushuru katika baadhi ya vitu vya kawaida kama vile mafuta ya kula, mkate na hata nepi za watoto.

Kamati ya fedha ya mipango ya kitaifa inapendekeza katika mswada wa fedha 2024 kuwekwa kwa ushuru wa 25% katika bidhaa za mafuta ya kula, hatua ambayo itapelekea bei ya bidhaa hiyo kuongezeka mara dufu.