Rais wa wasioamini katika uwepo wa Mungu ajitetea kuhudhuria hafla ya maombi ya kitaifa

Harrison Mumia alisema kwamba alipokea mwaliko wa kuhudhuria hafla hiyo ya maombi kutoka kwa bunge la kitaifa na kusisitiza kwamba hilo halibadili msimamo wake kuhusu Imani katika Mungu.

Muhtasari

• "natazamia mbele kufanya kazi na Wakristo, Wahindi, Waislamu katika kueneza mazungumzo ya Imani mbalimbali nchini,” aliongeza.

Rais wa muungano wa wasioamini katika uwepo wa Mungu, Harrison Mumia amejitetea vikali dhidi ya mashambulizi kutoka kwa watu baada ya kuhudhuria hafla ya staftahi ya maombi ya kitaifa Alhamisi katika mgahawa wa Safari Park jijini Nairobi.

Mumia alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri walioudhuria hafla hiyo ya maombi ya kitaifa ambayo hufanyika kila mwaka na kuongozwa na kiongozi wa taifa, Rais William Ruto.

Kupitia ukurasa wa X, awali ukijulikana kama Twitter, Mumia alitoa barua ya kufutilia mbali madai kwamba hatimaye amepata mwanga wa kuamini uwepo wa Mungu na kusema kwamba licha ya kuwepo katika maombi, bado anasalia kutoamini katika uwepo wa Mungu.

“Ningependa kuweka wazi kwamba mimi bado ni mtu asiyeamini katika Mungu, ukweli kwamba nilihudhuria hafla ya maombi ya kitaifa haimaanishi kwamba nimebadili mtazamo wangu wa kidunia,” Mumia alisema.

Aidha, Mumia aliweka wazi kwamba alipokea ombi la kuhudhuria katika maombi hayo kutoka kwa bunge la kitaifa, akisema kwamba hatua yake kualikwa licha ya kutoamini katika Mungu inaonyesha jinsi Kenya inajongea katika mkondo salama wa kutambua mitazamo mbalimbali.

“Mwalimu uliotumwa kwangu kuhudhuria maombi ya kitaifa kutoka kwa bunge la kitaifa ni hatua kubwa Kenya inapiga kuelekea uhuru na utambuzi wa Imani mbalimbali za kidini. Ishara hii inaonyesha jinsi Kenya iko katika njia salama ya kutambua desturi mbalimbali na kuzileta zote pamoja, ambapo watu wa Imani tofauti, wakiwemo wale wasioamini kwenye dini wanaweza kuja pamoja na kuwa na mazungumzo,” Mumia alisema.

“Kwa kuendelea kupigia debe huu mtazamo, Kenya inatarajiwa kuwa taifa lenye mfano wa jinsi nchi inaweza kushabikia umoja wa watu wake kutoka Imani tofauti, huku pia wakileta dhana ya mshikamano wa kitaifa. Tunatazamia mbele kufanya kazi na Wakristo, Wahindi, Waislamu katika kueneza mazungumzo ya Imani mbalimbali nchini,” aliongeza.