Matokeo rasmi ya uchaguzi Afrika kusini kutangazwa leo

Zoezi la kuhesabu kura linaingia katika hatua ya mwisho huku 98% ya matokeo yakiwa yamepokewa tayari.

Muhtasari
  • Chama tawala ANC kinatarajiwa kupoteza nguvu kilichoshikilia katika miongo mitatu ya siasa baada ya kupungua kwa wafuasi wake kwa kiwango kikubwa.

Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu Afrika kusini yanatarajiwa kutangazwa Jumapili jioni, afisa mmoja wa tume anasema.

Zoezi la kuhesabu kura linaingia katika hatua ya mwisho huku 98% ya matokeo yakiwa yamepokewa tayari.

Naibu mkurugenzi mtendaji wa tume ya uchaguzi nchini Mawethu Mosery, ameiambia televisheni ya eNCA kwamba tume itakesha usiku kucha Jumamosi kukabiliana na pingamizi na maombi.

Chama tawala ANC kinatarajiwa kupoteza nguvu kilichoshikilia katika miongo mitatu ya siasa baada ya kupungua kwa wafuasi wake kwa kiwango kikubwa.

Viongozi wa ANC wajadili njia ya kusonga mbele

Chanzo cha ANC chasema kuwa maafisa saba wakuu wa ANC, akiwemo Rais Cyril Ramaphosa wanakutana kujadili njia ya kusonga mbele baada ya matokeo ya uchaguzi.

Kama ilivyo kwa nchi nzima, jimbo tajiri zaidi la Afrika Kusini la Gauteng linatazamiwa kuwa na serikali ya mseto baada ya chama cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake.

Kwa 97% ya kura kukamilika kuhesabiwa, ANC imepata 35% tu ya kura – kupoteza kwa kiasi kikubwa tangu uchaguzi wa 2019 ilipopata 50%.

Bado ni chama kikubwa zaidi katika jimbo hilo, ambacho kinajumuisha jiji kubwa zaidi la Johannesburg na mji mkuu, Pretoria, lakini kitahitaji kuunda muungano.

Chama cha Democratic Alliance (DA) kiko katika nafasi ya pili, kwa asilimia 28 ya kura, kikifuatiwa na Economic Freedom Fighters (EFF) kwa asilimia 13%.

ANC imekuwa na wengi katika jimbo hilo tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.