Mbunge wa UDA Gabriel Kagombe kuzuiliwa kwa siku 5

Kagombe alikamatwa eneo la Kileleshwa siku tatu baada ya polisi kuanzisha msako wa kumsaka.

Muhtasari

• Kagombe alikamatwa Ijumaa 7,Juni 2024 baada ya ripoti ya DCI kuonyesha kuwa alihusika kwenye mauaji ya mawanaume mmoja kule Thika mwezi jana.

•David Nudati aliuawa kwa kupigwa risasi baada ya vurugu kutokea baina ya wafuasi wa mbunge wa Thika,Alice Wahome na MCA wa Kamenu,Peter Mburu.

Gabriel Kagombe
Image: Hisani

Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga hadi Ijumaa, Juni 7.

Kuzuiliwa kwake kulitangazwa mnamo Jumatatu, Juni 3, baada ya mbunge huyo kufikishwa mahakamani baada ya kudaiwa kuhusika katika kifo cha David Nudati,mwendesha bodaboda aliyepigwa risasi katika eneo la Thika mwezi jana.

Kagombe ambaye alifikishwa mbele ya mahakama katika Kaunti ya Machakos, atasomewa mashtaka yake Ijumaa kuhusiana na tukio la kupigwa risasi.

Akiwa katika Mahakama ya Machakos, Kagombe alikana mashtaka na kusababisha kuwekwa kizuizini.

Kagombe alikamatwa eneo la Kileleshwa siku tatu baada ya polisi kuanzisha msako wa kumsaka. Kukamatwa kwa mbunge huyo kumekuja baada ya askari wa upelelezi kufanya uchunguzi wa silaha zote zilizokuwa katika eneo la tukio mnamo siku hiyo ya mauaji na uchunguzi wa awali ulithibitisha kuwa anamiliki silaha iliyofyatua risasi hiyo.

Mbunge huyo alikuwa amehudhuria hafla ya kuzindua ujenzi wa soko mjini Thika wakati vita vilipozuka kati ya wafuasi wa mbunge wa Thika Alice Wahome na MCA wa Kamenu Peter Mburu.

Mapigano hayo yalisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa. David Nudati, mwanamume mwenye umri wa miaka 26 aliuawa kwa kupigwa risasi.

Baadaye maafisa wa DCI waliwaamuru wote waliokuwa na bunduki waliokuwepo wakati wa ghasia hizo kusalimisha bunduki zao katika makao yao makuu ya barabara ya Kiambu.

Wabunge wengine waliokuwepo wakati wa mzozo huo ni Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na mbunge wa Gatundu kaskazini Elijah Njoroge Kururia.