Wakazi wa Nairobi watahadharishwa kuhusu mvua ya wastani hadi kubwa

"Mvua ya wastani hadi kubwa huenda ikanyesha katika baadhi ya maeneo ya eneo la mji wa Nairobi," Kenya Met ilisema

Muhtasari

•Idara ya utabiri wa hali ya anga ilisema kuwa baadhi ya maeneo ya Nairobi ikiwemo Embakasi Mashariki yatapata mvua ya hadi milimita 20.

•Wataalamu hao wa hali ya hewa walisema maeneo mengine ya jiji la Nairobi pia yatapata mvua za wastani hadi nyingi.

Mvua
Image: MAKTABA

Wakaazi wa jiji la Nairobi wameshauriwa kutarajia mvua wa wastani hadi mvua kubwa katika utabiri wa hivi punde.

Idara ya utabiri wa hali ya anga ilisema kuwa baadhi ya maeneo ya Nairobi ikiwemo Embakasi Mashariki yatapata mvua ya hadi milimita 20.

Eneo la Westlands linatazamiwa kushuhudia mvua kubwa ya hadi milimita 100 huku eneo la Roysambu likipata mvua ya hadi 35mm.

Dagoretti Kaskazini itashuhudia mvua ya hadi 80mm huku Kibra ikipata mvua ya 60mm.

"Mvua ya wastani hadi kubwa huenda ikanyesha katika baadhi ya maeneo ya eneo la mji wa Nairobi," Kenya Met ilisema katika taarifa ya Jumanne jioni.

Wataalamu hao wa hali ya hewa walisema maeneo mengine ya jiji la Nairobi pia yatapata mvua za wastani hadi nyingi.

Katika kaunti ya Kiambu, eneo la Githunguri litapokea mvua ya hadi 100mm, Kiambaa (80mm), Limuru (60mm), Gatundu Kusini (20mm), Juja na Ruiru (10mm).

Katika kaunti ya Machakos, Mavoko itapokea mvua ya hadi 15mm, Kathianio (10mm), Masinga (10mm) na Machakos Town (5mm).

Siku ya Jumatatu, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya ilisema kuwa sehemu nyingi za nchi kwa ujumla zitakuwa kavu wiki hii.

Idara hiyp, hata hivyo, ilisema mvua inatarajiwa kunyesha katika maeneo machache ya nyanda za juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Victoria na Bonde la Ufa.

Kutakuwa na wastani wa halijoto ya juu mchana (kiwango cha juu) cha zaidi ya 30°C katika baadhi ya maeneo ya Pwani, Kaskazini-mashariki na Kaskazini-magharibi mwa Kenya, utabiri ulionyesha.

Idara hiyo ilisema kutakuwa na wastani wa halijoto wakati wa usiku chini ya 10°C katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa na Bonde la Ufa la Kati.

Watabiri waliwashauri Wakenya kutarajia hali ya baridi na mawingu mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, nyanda za chini kusini mashariki na Bonde la Ufa.

Kenya Met ilisema pepo zenye nguvu kutoka kusini hadi kusini-mashariki zenye kasi inayozidi knots 25 (12.9 m/s) zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Pwani, Kaskazini-mashariki na Kaskazini-magharibi mwa Kenya.

Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na Bonde la Ufa (Kisii, Nyamira, Nandi, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Siaya, Kisumu, Homabay, Busia, Migori, Narok, Baringo, Nakuru, Trans. -Nzoia, Uasin-Gishu, Elgeyo-Marakwet na Kaunti za Pokot Magharibi) zitakuwa na vipindi vya jua asubuhi ingawa maeneo machache huenda yakapata mvua ndogo, utabiri ulionyesha.

Mvua ya alasiri na usiku na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache na kusambaa sehemu kadhaa mara kwa mara.