Kwa nini Raila anaunga mkono azma ya DP Gachagua ya ‘One Man, One Vote, One Shilling’

Hata hivyo, ifahamike kwamba Gachagua si kwa kwanza kupendekeza mfumo huu wa ugavi wa rasilimali kwani ulipendekezwa kwenye mswada wa BBI ambao uliangushwa na mahakama mwaka 2022.

Muhtasari

• “Nataka kukubaliana na mfumo wa One Man One Vote One shilling. Ninakubaliana kabisa na hili,” Waziri Mkuu wa zamani aliambia mkutano wa wanahabari Alhamisi.

Ruto na Gachagua
Ruto na Gachagua
Image: X

Kinara wa upinzani Rala Odinga amezua joto la kisiasa nchini baada ya kuashiria kuunga mkono azma ya naibu wa rais wa ugavi wa mapato na rasilimali za taifa kulingana na idadi ya watu kimaeneo na wala si upana wa ardhi kimaeneo maarufu kama ‘One man, One vote, One shilling’.

Mfumo huu wa ugavi wa mapato ya serikali kimaeneo umekuwa ukipigiwa upatu na Gachagua na ilionekana kama mshangao mkubwa kwa wengi kuona Odinga, ambaye amekuwa hasimu mkuu wa kisiasa wa Gachagua tangu uchaguzi wa Agosti 2022 akimuunga mkono.

Odinga akizungumza na waandishi wa habari alasiri ya Alhamisi katika makao makuu ya chama cha ODM jijini Nairobi, alisema alikuwa tayari kufanya kazi na kila mtu nchini, akiwemo Gachagua, hata kama alikiri kuwa mfumo wa One Man One Vote One shilling haupendelewi na wengi.

“Nataka kukubaliana na mfumo wa One Man One Vote One shilling. Ninakubaliana kabisa na hili,” Waziri Mkuu wa zamani aliambia mkutano wa wanahabari Alhamisi.

Raila, ambaye ni kiongozi wa chama cha muungano cha Azimio La Umoja, alisema mfumo wa One Man One Vote One shilling kama ulivyopendekezwa wakati wa kongamano la Limuru 3 ulinaswa wakati wa Mpango wa Kujenga Madaraja na ulilenga kuhakikisha usawa katika maendeleo.

Cha kushangaza ni kwamba, Gachagua ni miongoni mwa waliopinga mfumo huu wa ugavi wa mapato na rasilimali za taifa kimaeneo, wakati ulipendekezwa kwenye mswada wa BBI na Odinga pamoja na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wanahisi kwamba Odinga anakubali kuunga mfumo huo mkono kwani kwa namna moja au nyingine unalenga kufufua malengo yaliyoazimiwa kwenye mswada wa BBI ambao ulituppwa nje na mahakama.