Rais Ruto amkabidhi Joel Ogolla zawadi kwa niaba ya marehemu babake, Francis Ogolla (video)

“Tunamuenzi kwa zawadi ya kitara, japo amefariki na tunamuomba bwana Joel Ogolla kujongea na kuipokea kwa niaba yake,” MC alisema kabla ya Joel kujongea na kukumbatiana na rais Ruto na baadae kukabidhiwa zawadi.

Muhtasari

• Hafla hiyo ilifanyika katika kituo cha majeshi ya Kenya cha Moi Airbase maeneo ya Eastleigh jijini Nairobi.

• Pia inaadhimisha huduma ya KAF kwa ubinadamu na matukio ya kihistoria hadi 2024.

Joe Ogolla apokea zawadi kwa niaba ya marehemu babake.
Joe Ogolla apokea zawadi kwa niaba ya marehemu babake.
Image: FACEBOOK//WILLIAM RUTO

Rais Ruto aliongoza hafla ya kuadhimisha miaka 60 tangu kitengo cha wanajeshi wa hewani cha Kenya kubuniwa.

Hafla hiyo ilifanyika katika kituo cha majeshi ya Kenya cha Moi Airbase maeneo ya Eastleigh jijini Nairobi.

Pia inaadhimisha huduma ya KAF kwa ubinadamu na matukio ya kihistoria hadi 2024.

Katika hafla hiyo, rais Ruto aliwatuza Wanajeshi mbalimbali kwa matendo yao mazuri ya kibinadamu kwa wananchi.

Pia hafla hiyo ambayo ilikuwa mahususi kwa jeshi la wanahewa waliweza kumtambua na kumuenzi aliyekuwa mmoja wao, marehemu Jenerali Francis Ogolla ambaye mpaka kifo chake mwezi Aprili mwaka huu katika ajali ya helikopta, alikuwa mkuu wa majeshi ya Kenya, CDF.

Mwanawe Joel Ogolla alijongea jukwaani na kukabidhiwa zawadi ya kumuenzi babake, baada ya kupatana na umauti akiwa katika majukumu yake ya kulitumikia taifa.

Katika hafla hiyo, mfawidhi alimuita Joel na kumtaka kupokea zawadi hiyo ya kumsherehekea babake baada ya kifo.

“Mheshimiwa rais, zawadi inayofuata ni ya marehemu Jenerali Francis Omondi Ogolla,” MC alisema kabla ya kuendelea kwa kutoa wasifu wake kwa ufupi jinsi alijiunga na kikosi cha jeshi 1984 hadi alipofariki 2024 Aprili.

“Tunamuenzi kwa zawadi ya kitara, japo amefariki na tunamuomba bwana Joel Ogolla kujongea na kuipokea kwa niaba yake,” MC alisema kabla ya Joel kujongea na kukumbatiana na rais Ruto na baadae kukabidhiwa zawadi kwa niaba ya babake.

Tazama tukio zima kwenye video hii hapa chini;