Jinsi serikali itaamua mchango wa kila mtu kwa SHIF - Nakhumicha

Waliosajiliwa chini ya NHIF watahitajika kuthibitisha maelezo yao.

Muhtasari

•Waziri huyo alisema serikali itazingatia kile alichokiita sifa za kiuchumi za kila Mkenya asiye na ajira au aliyejiajiri.

•"Ikiwa unaishi katika nyumba ya nyasi, haiwezi kujificha. Tutazingatia sifa za kiuchumi za wasio na ajira ili kuona jinsi watakavyochangia," Nakhumicha alisema.

Waziri wa afya Susan Nakhumicha
Image: twitter

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha amejitokeza kueleza jinsi serikali itakusanya michango kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).

Katika mahojiano na runinga ya Citizen Jumapili jioni, Nakhumicha alisema njia hiyo imeundwa mahususi kubainisha mapato ya kila mtu.

Waziri huyo alisema serikali itazingatia kile alichokiita sifa za kiuchumi za kila Mkenya asiye na ajira au aliyejiajiri ili kubaini jinsi watakavyolipa asilimia 2.75 ya mapato yao kwa hazina hiyo.

"Ikiwa unaishi katika nyumba ya nyasi, haiwezi kujificha. Tutazingatia sifa za kiuchumi za wasio na ajira ili kuona jinsi watakavyochangia," Nakhumicha alisema.

Akiongeza kuwa hii inajumuisha pesa ambazo mtu anapata ama kutuma kupitia simu.

Alifafanua zaidi kwamba wale ambao wamekuwa wakichangia NHIF wataona pesa zao zikihamishiwa SHIF, akiondoa hofu kwamba Wakenya huenda wakapoteza michango yao katika hatua hiyo mpya.

SHIF inatarajiwa kuanza katika muda wa wiki tatu zijazo, na Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua zoezi la usajili katika kipindi hiki.

Nakhumicha pia aliongeza kuwa Wakenya watahitajika kuthibitisha maelezo yao mara SHIF itakapotolewa.

"Waliosajiliwa chini ya NHIF watahitajika kuthibitisha maelezo yao. Sio usajili mpya, ni kuthibitisha maelezo tu. Wale ambao hawana maelezo ndio wajisajili," alisema.