Polisi wa Kenya wanatarajiwa kutua Haiti ndani ya wiki chache zijazo

Rais Ruto alielezea kuwa polisi wanatarajiwa kutumwa nchini Haiti hivi karibuni.

Muhtasari

•Rais Ruto amedokeza kuwa polisi wa Kenya wanatarajiwa kutumwa nchini Haiti ndani ya wiki zijazo ili kuimarisha usalama nchini humo na kukomesha magenge ya wahalifu.

•Kando na Kenya, nchi nyingine ambazo zimeonyesha nia ya kujiunga na misheni hiyo ni pamoja na Benin, Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad.

Image: BBC

Rais Ruto amedokeza kuwa polisi wa Kenya wanatarajiwa kutumwa nchini Haiti ndani ya wiki chache zijazo.

 Licha ya changamoto za mahakama kuchelewesha misheni ya kutumwa kwa  polisi nchini Haiti,Rais Ruto ameweka wazi kuwa ndani ya wiki chache, polisi wa Kenya watakuwa wanatumwa  nchini humo  kukomesha wahalifu na makundi ya magenge ambayo yamekuwa yakiwahangaisha watu.

Kenya inalenga kuongoza misheni inayoungwa mkono na umoja wa mataifa ili kulilinda taifa la Haiti, lililokumbwa na ghasia, umaskini na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.Kenya imeratibiwa kutuma maafisa  takriban 1,000 kwa misheni hiyo pamoja na wafanyikazi kutoka nchi zingine kadhaa.

Rais Ruto alizuru katikati mwa Kenya siku ya Jumapili huku akidai kuwa polisi wa Kenya wako tayari kwa shughuli hio;

"Watu wa Haiti labda wanangojea, kwa neema ya Mungu, kwamba labda kufikia wiki ijayo au wiki nyingine, tutatuma maafisa wetu wa polisi kurejesha amani," Rais Ruto alisema.

Azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa mwezi Oktoba mwaka jana liliidhinisha ujumbe huo lakini mahakama ya Kenya mwezi Januari ilichelewesha kutumwa. Mahakama ilisema kuwa serikali haikuwa na mamlaka ya kutuma maafisa wa polisi nje ya nchi bila makubaliano ya awali.

Serikali ilipata makubaliano hayo mnamo Machi 1 na rais  Ruto aliambia BBC mwezi uliopita kwamba alitarajia jeshi la Kenya kwenda Haiti ndani ya wiki kadhaa.

Aidha chama kidogo cha upinzani nchini kiliwasilisha kesi mpya kujaribu kuzuia. Mahakama kuu ya Kenya inatazamiwa kuangazia kesi hiyo Juni 12. Kando na Kenya, nchi nyingine ambazo zimeonyesha nia ya kujiunga na misheni hiyo ni pamoja na Benin, Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad.