Uhuru anapaswa kuwa na subira-Mbunge Koech

Sh28m ambayo ofisi ilipokea ilikuwa mwaka wa 2022/2023 wakati bunge lilitenga Sh655 milioni kwa ofisi yake.

Muhtasari
  • Akiongea kwenye runinga ya Citizen siku ya Jumanne, Koech alitaja hatua ya ofisi ya rais wa zamani kufafanua suala hilo kuhusu bajeti yake kuwa kubwa na ya kisiasa.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech amemtaka rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa na subira na kuepuka kuibua hisia kuhusu mgao wa bajeti kwa ofisi yake.

Akiongea kwenye runinga ya Citizen siku ya Jumanne, Koech alitaja hatua ya ofisi ya rais wa zamani kufafanua suala hilo kuhusu bajeti yake kuwa kubwa na ya kisiasa.

"Nitasema hivi, ofisi ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta iwe na subira. Watapata pesa zao. Hakuna haja ya kuigiza," akasema.

Koech alisema serikali si ndogo na itampa rais huyo wa zamani manufaa yake.

"Nilisema kwamba serikali hii si ndogo. Haitamfanyia Uhuru Kenyatta kile ilichomfanyia William Ruto," alisema na kuongeza kuwa rais huyo wa zamani hajanyimwa ujira wake.

"Ni nini cha haraka sana kwamba lazima tuhudumie rais ambaye yuko vizuri?"  Aliuliza.

Mbunge huyo aliongeza kuwa kila Mkenya anakabiliwa na nyakati ngumu za kiuchumi na kuongeza kuwa rais huyo wa zamani hapaswi kuwa ubaguzi.

Mbunge huyo alipingana na kuendelea kwa Rais huyo wa zamani kujihusisha na siasa akiwa mwenyekiti wa Azimio na kiongozi wa chama cha Jubilee akisema huo ni ukiukaji wa sheria.

Matamshi ya mbunge huyo yanajiri baada ya afisi ya Uhuru kukashifu serikali kwa kutoheshimu haki zake za kikatiba kwa mujibu wa sheria za marupurupu ya kustaafu.

Msemaji wa Uhuru Kanze Dena alisema ofisi hiyo imenyimwa bajeti na ilipokea Sh28m pekee katika mwaka uliopita wa kifedha licha ya afisi hiyo kutengewa zaidi ya Sh1 bilioni.

Sh28m ambayo ofisi ilipokea ilikuwa mwaka wa 2022/2023 wakati bunge lilitenga Sh655 milioni kwa ofisi yake.

Haya yanajiri kufuatia shutuma zilizotolewa na afisi ya rais huyo wa zamani siku ya Jumatatu, ikishutumu hali ya kupuuza afisi yake na hivyo kumlazimisha kulipa bili.

Kwa mujibu wa shutuma zilizotolewa na ofisi ya rais huyo wa zamani, katika mwaka wa 2022/2023 bunge lilitenga milioni 655 kwa ofisi yake ambapo milioni 28 tu ndio zimehesabiwa.