Mabadiliko kamili kutoka bima ya Afya (NHIF) hadi mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) yamepangwa kuanza Julai 1, 2024.
Wizara ya afya itaongoza harakati kubwa ya usajili katika kaunti zote 47, kuanzia Juni 21 ili kuwezesha mabadiliko hayo.
Katika ujumbe kufuatia mkutano wa baraza la mawaziri uliofanyika siku ya Jumanne 12,Juni 2024,serikali iliwataka wakenya wote kushiriki zoezi hilo, ambalo linalenga kujumuisha Kenya miongoni mwa mataifa yenye huduma ya afya kwa wote.
"Wakenya wanaweza kujiandikisha kwa simu, katika hospitali zote za umma,ambapo tumeeka takriban wahudumu 100,000 kote nchini..."
Hazina hiyo mpya ya afya itashuhudia nchi ikivuka kikamilifu kutoka kwa mfumo wa sasa wa NHIF, huku kila mkenya akihitajika kuchangia asilimia 2.75 ya mapato yake kwa hazina hiyo.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema kuwa serikali itazingatia hali ya kiuchumi ya wakenya wasio na ajira au waliojiajiri ili kubaini michango yao kwa hazina hiyo.
Mwanzoni mwa mwaka ,waziri wa afya alielezea sababu za kuondoa NHIF na kubadili hadi SHIF.Nakhumicha,alifichua kuwa mfumo wa NHIF ulikumbwa na kasoro nyingi za kimsingi ambazo ziliufanya kuwa chaguo la matibabu lisiloweza kuepukika kwa wakenya, hivyo basi haja ya kubadili.
Waziri huyo aidha aliongeza kuwa NHIF haitoi huduma kamili ya matibabu ya baadhi ya magonjwa kama Saratani, na hivyo itawaacha wakenya wagonjwa na bili za matibabu baada ya kuendelea.
Pia alibainisha kuwa NHIF haishughulikii magonjwa yanayopatikana wakati wa kuzaliwa, wala kushughulikia uchunguzi wa jumla, ambao mfumo mpya unalenga kubadilika.