Uingereza kutoa Ksh.82M kusaidia miradi ya miundo msingi ya Kenya

Waziri mkuu wa Uingereza,Rishi Sunak alisema kuwa Uingereza imejitolea kuendesha mfumo mzuri zaidi wa kimataifa ambao unaboresha maisha ya watu kote ulimwenguni.

Muhtasari

•Waziri mkuu wa Uingereza alikuwa akizungumza wakati wa mkutano  mjini Apulia, Italia ambao ulihudhuriwa na Rais William Ruto.

• Alisema Uingereza imejitolea kuendesha mfumo mzuri zaidi wa kimataifa ambao unaboresha maisha ya watu kote ulimwenguni.

Rais Ruto na Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak
Image: Hisani

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ametangaza mchango wa Sh82 milioni kwa Kenya ili kuboresha miundo mbinu nchini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa, Sunak alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kupanga, kuweka vipau mbele na utekelezaji wa mipango ya miundo mbinu kati ya Uingereza, Kenya na nchi nyingine saba zenye umaarufu kiuchumi.

"Tukiangazia miradi ya uchukuzi iliyochaguliwa kutoka kwa mpango wa kukuza viwanda, ushirikiano huu wa kibunifu utasababisha ushirikiano wa karibu na serikali ya Kenya kuhusu miundo mbinu ya kimkakati na uwekezaji na ni ushirikiano wa kwanza kati ya ushirikiano wa nchi saba zilizoendelea kiuchumi..." Sunak alisema.

Vile vile ,Sunak alisema kuwa Uingereza imejitolea kuendesha mfumo mzuri zaidi wa kimataifa ambao unaboresha maisha ya watu kote ulimwenguni.

Waziri mkuu Sunak pia alielezea umuhimu wa kusaidia nchi katika kuwasilisha mabadiliko yao ya nishati safi na fursa za kujiinua zinazowasilishwa na akili ya mitambo.

"Ukuzaji wa akili ya mitambo almaarufu AI ,ni sehemu kuu na ufadhili uliotangazwa leo utasaidia kuhakikisha kuwa mabadiliko haya ya mitetemo yanatokea kwa njia ambayo inafanya kazi kwa wote," alisema.

Waziri mkuu alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa shirika la kiserikali linalojumuisha mataifa saba yenye uchumi mkubwa huko Apulia, Italia. Rais Ruto ambaye alisafiri hadi Italia Alhamisi jioni alihudhuria.

Mkutano huo unalenga kutoa jukwaa la mijadala ya hali ya  juu ya mada zinazovutia kimataifa kama vile usalama wa nyuklia, uhuru wa usalama wa chakula na masuala ya kibinadamu.

Pia inataka kujenga maelewano ya pamoja katika ngazi ya juu zaidi ya kisiasa kwa ajili ya amani ya kina, ya haki na ya kudumu nchini Ukraine kwa kuzingatia mkataba wa umoja wa mataifa.

Zaidi ya hayo, mkutano huo utaanzisha mchakato wa kuelekea amani kwa kujadili kwa mara ya kwanza katika ngazi ya juu ya kisiasa, ramani ya jinsi ya kushirikisha pande zote mbili katika mchakato huo.