Kwa nini Wabunge wanapaswa kukataa Mswada wa Fedha- Gideon Moi

Aliendelea kusema kuwa wataalam wa Uchumi wanakubali kwamba Kenya haikabiliwi na tatizo la mapato bali ni suala la matumizi.

Muhtasari
  • Seneta huyo wa zamani alibaini kuwa wakati baadhi ya ushuru wa adhabu umeondolewa, zingine za kuadhibu zimeingizwa kimya kimya kwenye Mswada huo.
Gideon Moi
Image: MAKTABA

Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi sasa anasema kuwa Wabunge wa Kenya lazima wakatae Mswada wa Fedha wa 2024.

Katika taarifa ya Alhamisi, Moi alisema kuwa majaribio yoyote ya kuongeza ushuru ili kukabiliana na nakisi ya bajeti yanaweka mzigo usio wa lazima kwa Wakenya.

Aliendelea kusema kuwa wataalam wa Uchumi wanakubali kwamba Kenya haikabiliwi na tatizo la mapato bali ni suala la matumizi.

Seneta huyo wa zamani alibaini kuwa wakati baadhi ya ushuru wa adhabu umeondolewa, zingine za kuadhibu zimeingizwa kimya kimya kwenye Mswada huo.

“Kwa hiyo, Bunge la Kitaifa linapaswa kuukataa Mswada wa Fedha wa 2024 kwa ujumla wake.

"Marekebisho yaliyopendekezwa ya vipengee vya mswada unaoelezea hatua za kutoza ushuru ambazo hazikubaliki sana yameghairiwa na mapendekezo mengine ya kuadhibu yaliyoingizwa kwenye mswada huo," Moi alisema.

Kiongozi huyo wa chama cha Kanu alibainisha kuwa ili kufikia ustawi, uongozi wa nchi lazima utangulize maendeleo ya viwanda badala ya ushuru.

Alisema hii itasaidia kupanua wigo wa kodi na hivyo wataweza kukuza ukusanyaji wa mapato.

"KRA ilikosa kufikia makadirio ya mapato yake ya ushuru licha ya hatua kali za kutoza ushuru zilizoletwa na Mswada wa Fedha wa 2023, kuonyesha kwamba viwango vya juu vya ushuru sio lazima visababishe mapato ya juu ya ushuru.

"Ili kufikia ustawi wa kiuchumi, Kenya lazima itangulize ukuaji wa viwanda badala ya ushuru ili kupanua wigo wa ushuru."

Wiki jana, Moi alionya kuwa Mswada wa Fedha, 2024 utawahukumu Wakenya zaidi katika umaskini ikiwa mapendekezo ya ushuru hayatarekebishwa.