Maduka yafungwa, usafiri kulemazwa huku maandamano Kisumu yakianza

"Hatutachoka kuandamana ,huu ni wakati wetu na tutawafundisha somo..." Alifoka kijana mmoja

Muhtasari

•Biashara katika mji  huo zilibaki zikiwa zimepooza, huku maduka yakiwemo maduka makubwa yaliyokuwa yamefunguliwa mapema yakifungwa saa 9 asubuhi.

•Usafiri pia uliathirika pakubwa, huku magari machache yakionekana kukwama barabarani.

kundi la vijana wakiandamana kule kisumu,Jumanne Juni 25 2024
kundi la vijana wakiandamana kule kisumu,Jumanne Juni 25 2024
Image: Faith Matete

Waandamanaji wa kupinga mswada wa fedha mjini Kisumu walimiminika katika mitaa mbalimbali ya Jiji kuunga mkono mwito wa 'Kataa Mswada wa Fedha'.

Waandamanaji waliokuwa na amani walivamia barabara za jiji la kando ya ziwa wakiwa na mabango, nyimbo, densi na kuimba nyimbo za kumpinga Rais William Ruto.

Vijana hao walikuwa wamekusanyika katika viwanja vya Kondele mapema saa tisa alfajiri ambapo walianza kusonga mbele kwa makundi na hatimaye kuanza maandamano.

“Hatutachoka kuandamana, huu ni wakati wetu na tutawafundisha somo,” alifoka kijana mmoja.

Biashara katika mji huo zilibaki zikiwa zimepooza, huku maduka yakiwemo maduka makubwa yaliyokuwa yamefunguliwa mapema yakifungwa saa 9 asubuhi.

Usafiri pia uliathirika pakubwa, huku magari machache yakionekana kukwama barabarani. Maafisa wa polisi waliwafuatilia waandamanaji barabarani.