Kikosi cha kwanza cha maafisa wa polisi wa Kenya takriban 400 kimeelekea nchini Haiti baada ya kusafiri usiku wa Jumatatu ,Juni 24 2024.
Maafisa hao ambao awali walikuwa wamekusanyika katika chuo cha mafunzo cha polisi cha Embakasi kwa taarifa ya kabla ya kutumwa waliondoka JKIA saa 7 usiku kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya (KQ).
Wanatarajiwa kuwasili Port-au-Prince leo kabla ya kuanza kwa misheni yao. Walionwa na Katibu wa baraza la mawaziri wa mambo ya ndani Kindiki Kithure, katibu mkuu Raymond Omollo na Inspekta Jenerali Japhet Koome.
Pia alikuwepo mkurugenzi mkuu mtendaji wa KQ Allan Kilavuka miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa polisi. Hapo awali, Rais William Ruto ambaye pia alikuwepo wakati wa kikao cha taarifa hiyo aliwakabidhi maafisa hao bendera ya Kenya.
Kithure alitoa shukrani zake kwa shirika la ndege la Kenya Airways kwa kuwezesha uchukuzi wa maafisa hao.