Waziri wa utumishi wa umma, utendakazi na usimamizi, Moses Kiarie Kuria ametangaza rasmi vita dhidi ya naibu wa rais Rigathi Gchagua katika kile kinachoonekana kuwa ni mzozo wa ubabe wa kisiasa eneo la Mlima Kenya.
Kuria kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X amekuwa akimshambulia DP Gachagua kwa kumtuhumu kwa mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika katika eneo pana la Mlima Kenya.
Siku chache baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z wanaopinga kupitishwa kwa mswada wa fedha wa 2024 kufanyika katika angalau kaunti 30, zikiwemo kaunti za Mlima Kenya, Moses Kuria sasa amejitokeza kumtuhumu DP Gachagua kwa ghasia hizo.
Kwa mujibu wa Kuria, DP Gachagua ndiye yuko nyuma ya ghasia hizo zilizoshuhudiwa katika baadhi ya kaunti za Mlima Kenya na kupelekea kuharibiwa kwa mali ya umma.
Kuria alisema kwamba yeye huenda akawa anatofautiana na rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa masuala mbalimbali lakini Kenyatta hajawahi fikia hatua ya kufadhili ghasia katika eneo hilo.
“Nina tofauti zangu za maoni na mtindo na rafiki yangu Uhuru Kenyatta. Lakini kwa miaka yote niliyomfahamu hajawahi kufadhili vurugu katika eneo la Mlima Kenya,” Kuria alisema.
Jumanne, kulishuhudiwa ghasia na kuharibiwa kwa mai katika kaunti za Laikipia, Embu na hata kaunti ya nyumbani ya Gachagua, Nyeri, vurugu ambazo Kuria anadai zilikuwa na mchango wa naibu wa rais.
Alitangaza kwamba sasa ni vita baina yake na Gachagua, akitumia msemo wa Kiluhya kwamba watapambana Omundu Khu Mundu.
“Ni mimi na yeye sasa Omundu Khu Mundu. Kari gani?!” Kuria alisema.
Tofauti za wawili hao zimekuwa zikishuhudiwa tangu Gachagua alipoweka wazi kwamba anaunga mkono ugavi wa rasilimali za kitaifa kulingana na idadi ya watu, maarufu kama One Man One Vote One Shilling, jambo ambalo lilivutia pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo.