•Kifo cha Mutegi kilithibitishwa na familia yake ambao walimsifu kama mtu mkarimu ambaye alijawa na ucheshi.
•Alikuwa mchambuzi mkazi kwenye kipindi cha ‘Cheche’ cha power breakfast cha Citizen TV.
Mtangazaji wa zamani wa runinga ya Citizen na gwiji wa vyombo vya habari,Mutegi Njau ameaga dunia.
Mutegi alifariki Juni 27, baada ya kupata kiharusi wiki kadhaa kilichosababisha kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Kifo cha Mutegi kilithibitishwa na familia yake ambao walimsifu kama mtu mkarimu ambaye alijawa na ucheshi.
"Hakuwa tu msingi wa familia yetu bali pia mtu wa kupendwa sana katika jamii yetu. Kwa sasa tupo katika maandalizi ya mazishi yake na tutakuletea habari ndani ya siku moja au mbili zijazo. Uwepo wako ungethaminiwa sana tunapokusanyika. kuheshimu kumbukumbu yake," ilisema taarifa hiyo.
Familia yake ilisema Mutegi alifariki kwa amani Alhamisi jioni mwendo wa saa saba usiku.
"Baba alikuwa mtu wa ajabu ambaye ukarimu wake, hali ya ucheshi, na kujitolea kwa kazi yake kuliacha athari ya kudumu kwa kila mtu aliyekutana naye," ilisoma sehemu ya taarifa ya familia.
Mutegi, ambaye taaluma yake ya utangazaji ilidumu kwa miongo kadhaa, alifanya kazi katika mashirika mashuhuri ya vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Royal Media Services. Alikuwa mchambuzi mkazi kwenye kipindi cha ‘Cheche’ cha power breakfast cha Citizen TV.
Wakati huo huo, mwandani wake wa zamani David Makali aliingia kwenye mitandao ya kijamii kumkumbuka Mutegi.
"Nimehuzunishwa na kufariki kwa mfanyakazi mwenza mkuu, mwenyeji mwenza na mwanajopo Mutegi Njau. Kazi yako katika dunia hii na ipate thawabu na kumbukumbu yako idumu milele miongoni mwa wale uliowashauri na kuwapa vipawa, au waliofurahia wema wako,” Makali alisema.
Safari yake katika vyombo vya habari ilianza mwaka wa 1979, huku mapenzi yake yakichanua tangu enzi za rais mwanzilishi wa kenya mzee Jomo Kenyatta.