Serikali imeahidi kuzuia uhalifu au uharibifu unaopangwa kutokana na maandamano ya kuipinga serikali yanayoendelea kote nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kenya Kithure Kindiki alikashifu ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kitaifa siku ya Jumanne, akidai kuwa zilisababisha machafuko, kuharibu mali ya umma, na kulemaza uchukuzi katika baadhi ya kaunti ambako maandamano yalifanyika.
Waziri Kindiki alisema kuwa baadhi ya wahalifu waliojifanya waandamanaji waliingilia maandamano ya amani ili kupora, kuharibu mali na kusababisha machafuko ya umma.
Huku akirejelea maandamano yaliyopangwa kufanyika wiki nzima, CS Kindiki alitoa onyo kali kwa wahusika, akisema kuwa vyombo vya usalama vitazuia visa hivyo kwa gharama yoyote.
"Licha ya kusitishwa kwa Mswada huo, makundi ya wahalifu wanaovamia watu yanaendelea kuwa hatari kubwa kwa umma, wakiendesha mipango iliyotangazwa ya maandamano ya amani ya kuvuruga utulivu wa umma, kuchoma moto, kuzuia usafiri wa umma na kutisha watu wa Kenya kwa vurugu, ”alisema CS.
"Waandalizi wa ghasia za leo katika maeneo ya Nairobi, Mombasa na sehemu nyingine kadhaa za Nchi wanaripotiwa kupanga kurudia machafuko na uporaji wao wa kikatili tena Alhamisi na Jumapili wiki hii, na pengine mara nyingi zaidi katika siku zijazo."
“Utawala huu wa ugaidi dhidi ya watu wa Kenya na kutoadhibiwa kwa magenge hatari ya uhalifu lazima ukomeshwe kwa gharama yoyote ile. Serikali imedhamiria kuwakomesha wahalifu wanaolenga kutishia umma na kudhuru Kenya, licha ya majaribio ya kuingiza uhalifu kisiasa.”
Kulingana na Waziri Kindiki, kuna wafadhili na wapangaji wa maandamano hayo ambao hawakutajwa majina ambao alihakikishia umma kwamba watashukuliwa hatua.
Alisema kuwa maandamano hayo yamechochewa kisiasa na kwamba serikali itashughulikia suala hilo.
"Baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa ushahidi unaoendelea, Serikali inawahakikishia wananchi kwamba wapangaji, watekelezaji na wafadhili wa matukio ya uchomaji moto mkubwa, ujambazi wa kutumia nguvu na uhalifu mwingine wa kikatili watafikishwa mahakamani," alisema.
Kindiki pia aliwapongeza wasimamizi wa sheria kwa jinsi wanavyoshughulikia waliofanya fujo huku akibainisha kuwa waliendelea kuwa watulivu licha ya fujo kuwa mingi.
Aliviagiza vyombo vya usalama kuzuia majaribio yoyote yajayo ya ghasia kwa gharama yoyote ile, pamoja na maandamano ya kusaidia kulinda maisha na mali, huku pia akibainisha kuwa maafisa wanaotuhumiwa kwa mauaji watakabiliwa na mashtaka ya kisheria.
“Polisi wanaendelea kufanya kazi kwa weledi na kwa utulivu katika kudhibiti hali za uchochezi zinazojitokeza wakati wa ghasia hizo.
Serikali inawapongeza maafisa wote wa kutekeleza sheria wanaoendelea kutekeleza majukumu yao magumu ya kuzuia uhalifu na kulinda maisha na mali ya Wakenya.
Madai ya baadhi ya matukio ya utendakazi usio halali wa maafisa wa kutekeleza sheria yatachunguzwa na hatua zinazofaa kuchukuliwa,” Kindiki alisema.
"Vyombo vya usalama vinaendelea kuwa macho kuzuia madhara kwa umma na kujaribu kushambulia miundombinu muhimu na nembo za uhuru wetu."