Sonko ajibu madai ya kununua majeneza katika maandamano siku ya Jumanne

Mike Sonko aliwataka wale wanaomshtaki kwanza kuangalia ni wapi na nani walinunua majeneza hayo

Muhtasari

•Haya yanajiri baada ya wanasiasa kusemekana kuwakodi wahuni kutoka maeneo ya ghetto maarufu jijini Nairobi kupora na kusababisha uharibifu jijini wakitarajia kuwalaumu waandamanaji wa Gen Z.

•Sonko alikanusha kuwa alimlipa mtu yeyote wala hakununua majeneza yaliyotolewa  kwenye ‘maandamano’ ya Jumanne.

Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amekanusha vikali madai ya kufadhili ununuzi wa majeneza yaliyosafirishwa katikati mwa jiji la Nairobi sku ya Jumanne.

Akijibu madai haya kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Sonko alikanusha kuwa alimlipa mtu yeyote wala hakununua majeneza yaliyotolewa  kwenye ‘maandamano’ ya Jumanne.

"Nimeona kuna watu, wanaopenda kunichafulia jina kwa kueneza propaganda  na kusema uongo na akili zao feki ati mimi ndiye niliyepanga watu kupora kwenye CBD na majeneza yaletwe CBD pia,” sehemu ya chapisho lake ilisema.

Mike Sonko alionyesha kuwaunga mkono GenZ ambao waliingia barabarani kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Alidhihirisha kupitia machapisho kadhaa ambapo alizungumza juu ya umuhimu wa serikali kusikiliza vijana ambao ni siku zijazo lakini hakuwahi kuungana nao mitaani kwa maandamano.

Usaidizi wake hata hivyo umemuacha katika wakati mgumu baada ya kusemekana kuwa alikuwa miongoni mwa wabunge hao ambao walilipa pesa wahuni kupora maduka na vibanda vya Nairobi CBD bila kusahau masanduku mengi yaliyoonyeshwa kwenye barabara ya Moi Avenue tarehe 2 Julai 2024.

Katika utetezi wake, Mike Sonko aliwataka wale wanaomshtaki kwanza kuangalia ni wapi na nani walinunua majeneza hayo tangu yanunuliwe CBD.

Pia aliomba namba za lori la bluu lililokuwa likiwasafirisha zikaguliwe kabla hawajamshtaki kwa kuwafadhili.

Mike Sonko aliendelea kumnyooshea vidole mwanaharakati ambaye anasema ni adui yake mkubwa kama mmoja wa watu walioonekana kwenye kanda za CCTV wakiwa wamebeba majeneza hayo.

“Hapa kuna ukweli sahihi Majeneza yalinunuliwa ndani ya jiji. Walisafirishwa hadi CBD katika canter ya bluu. Baadhi ya wanaharakati wanaojulikana, mmoja wao, adui yangu mkubwa, hata alinaswa moja kwa moja kwenye kamera akiwa amebeba majeneza hayo.” Aliandika.

Haya yanajiri baada ya wanasiasa kusemekana kuwakodi wahuni kutoka maeneo ya ghetto maarufu jijini Nairobi kupora na kusababisha uharibifu jijini wakitarajia kuwalaumu waandamanaji wa Gen Z.