Nyamira: Mwanamke asakwa kwa madai ya kumdunga kisu mumewe hadi kufa

Haijabainika ni kwa nini wanandoa hao walikuwa wakizozana kuhusu ng'ombe wao.

Muhtasari

• Ilithibitishwa  kuwa marehemu na mkewe walikuwa wamepigana nyumbani kuhusu ng'ombe aliyenunuliwa na mwanamke kabla ya kudungwa shingoni.

•Kisa hicho kilishuhudiwa Julai 7,2024 katika kijiji cha Gesima, Kaunti ya Nyamira.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Mwanamke mmoja yuko mafichoni baada ya kudaiwa kumdunga kisu na kumuua mumewe katika vita vya kinyumbani kuhusu ng'ombe wao katika kijiji cha Gesima, Kaunti ya Nyamira.

Mwili wa Francis Otiso, 43, ulipatikana nyumbani kwao ukiwa na kisu shingoni. Tukio hilo lilitokea Jumapili Julai 7 asubuhi.

Mwili huo, kwa mujibu wa polisi ulipatikana ukiwa kwenye dimbwi la damu ukiwa na majeraha yanayoonekana shingoni. Ilithibitishwa kuwa marehemu na mkewe walikuwa wamepigana nyumbani kuhusu ng'ombe aliyenunuliwa na mwanamke.

Mapigano hayo yalimfanya mwanamke huyo kuokota kisu cha jikoni ambacho alitumia kumchoma shingoni mumewe na kumuua papo hapo. Haijabainika ni kwa nini wanandoa hao walikuwa wakizozana kuhusu ng'ombe wao.

Kulingana na polisi, mshukiwa alitoroka eneo la tukio alipoona  wananchi wakija kwake. Aliogopa kwamba angeuawa. Kisu cha jikoni chenye madoa ya damu kilipatikana katika eneo la tukio. Polisi walisema walikuwa wakimsaka mwanamke huyo  ili kumhoji.

Mwili huo ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kibinafsi ya Gucha ukisubiri uchunguzi wa maiti.