Polisi wamkamata mwanamume aliyekuwa akisafirisha kilo 146 za bangi

Mshukiwa huyo alikamatwa kwenye babarabara kuu ya KIsii -Migori huku dereva aliyekuwa naye akitoroka.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alikamatwa Julai 7,2024 wakati alipokuwa akisafirisha bangi baada ya kujaribu kuwahepa polisi huku gari alilokuwa nalo likizuiliwa.

• Polisi wanazuilia gari hilo pamoja na bangi  katika kituo cha polisi cha Kisii Central wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa mshukiwa.

Polisi wamemkamata mshukiwa mmoja  aliyekuwa akisafirisha kilo 146 za bangi kwenye barabara kuu ya Kisii-Migori.

Kulingana na ripoti ya polisi, mshukiwa kwa jina Collins Otieno alinaswa katika tukio la kuwinda gari mnamo Jumapili, Julai 7, 2024.

Polisi ambao walikuwa wakishika doria kwenye barabara ,walikuwa wameweka kizuizi katika eneo la Iyabe-Bomokara ambapo walinasa gari aina ya  Toyota Land Cruiser TX yenye nambari ya usajili KDG 508E pamoja na watu wawili waliokuwa ndani yake.

Dereva huyo aliondoka kwa kasi katika harakati za kuwatoroka  polisi waliokuwa wameanza kufanya upekuzi kwenye gari hilo na kusababisha msako mkali wa gari.

Msako huo haukudumu kwa muda mrefu kwani gari la waliotoroka lilishindwa kulidhibiti na kukwama kwenye mtaro, na kusababisha kukamatwa kwa mmoja wa watu waliokuwa ndani, Collins Otieno mwenye umri wa miaka 42, huku dereva akifanikiwa kutokomea kwenye vichaka vilivyokuwa karibu.

Magunia sita ya bangi yakiwa yamefichwa ndani ya gari yalipatikana huku yakiwa  yamehifadhiwa ndani ya begi ya kubebea mizigo.

Polisi wanazuilia gari hilo pamoja na bangi  katika kituo cha polisi cha Kisii Central wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa mshukiwa.

"Mshukiwa alisindikizwa hadi Kituo cha polisi cha Suneka kwa shughuli zaidi, huku mihadarati iliyonaswa na gari hilo vikizuiliwa katika kituo kikuu cha polisi cha kisii kama vielelezo," polisi walisema.

Polisi wamezidisha msako wa kumtafuta dereva aliyetoroka.