Wanafunzi madaktari bado wamepiga kambi nje ya Afya House

Wamesema wanataka wapate kuajiriwa mara moja kwa mujibu wa CBA

Muhtasari

•Hali hii ilikuwa kama mbinu mojawapo ya kushinikiza serikali kuwaajiri wanafunzi  madaktari wanaofanya mafunzo ya vitendo kulingana na Mkataba wa Makubaliano (CBA) wa mwaka 2017.

•‘Nakhumicha must go!’, ndivyo baadhi ya mabango yalisomeka huku yakimrejelea Waziri wa Afya Susan Nakhumicha.

•Wafanyakazi wengine wa afya walionekana wakiwa wamelala kwenye mifuko ya kulalia nje ya jengo hilo.

Madaktari walala nje ya Afya House baada ya siku mrefu ya maandamano
Image: HISANI

Wanafunzi wa mafunzo ya udaktari walipiga kambi nje ya makao makuu ya Wizara ya Afya katika Afya House, Nairobi, usiku wa kuamkia leo baada ya siku ya maandamano mnamo Jumatatu.

Hali hii ilikuwa kama mbinu mojawapo ya kushinikiza serikali kuwaajiri wanafunzi  madaktari wanaofanya mafunzo ya vitendo kulingana na Mkataba wa Makubaliano (CBA) wa mwaka 2017.

Wafanyakazi wa afya walitumia muda mwingi wa Jumatatu wakifanya maandamano nje ya makao makuu ya Wizara ya Afya katika eneo la Upper Hill.

Ilipowadia jioni, waliwasha mishumaa na taa ili kuendelea na maandamano majira ya usiku licha ya mvua nyepesi iliyokuwa ikinyea jijini.

Video zilizoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maafisa wa afya wakiimba wimbo wa taifa huku wakipeperusha bendera za Kenya huku wakiwa wamebeba mabango.

‘Nakhumicha must go!’, ndivyo baadhi ya mabango yalisomeka huku yakimrejelea Waziri wa Afya Susan Nakhumicha.

Wafanyakazi wengine wa afya walionekana wakiwa wamelala kwenye mifuko ya kulalia nje ya jengo hilo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno cha Kenya (KMPDU), Davji Atellah, alisema awali kwamba chama hicho kilikuwa kimendesha misururu ya mikutano ili kutekeleza mpango wa kurejea kazini katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Wizara ya Afya.

Kwa mujibu wa Atellah, suala la upangaji wa mafunzo ya vitendo lilipaswa kutatuliwa ndani ya siku 60 kama ilivyoainishwa kwenye CBA ya mwaka 2017.

“Kama tunavyojua sote, siku 60 zinaisha tarehe 7 Julai 2024. Hadi sasa tumekubaliana na Wizara ya Afya kwamba wanafunzi wa mafunzo ya vitendo lazima wawekwe kwenye vituo vya kazi kulingana na CBA ya mwaka 2017 kabla ya kumalizika kwa dirisha la mazungumzo la siku 60 kama ilivyo kwenye mpango wetu wa kurejea kazini,” Atellah alisema wakati huo.

“Wizara ya Afya inapaswa kufanya mazungumzo na Hazina ya Kitaifa kabla ya mkutano wetu wa mwisho uliopangwa kufanyika Alhamisi, tarehe 4 Julai 2024.”