Kenya ni taifa la kidemokrasia, Ruto awajibu wanaotaka ajiuzulu

Ruto alieleza kuwa Kenya ni nchi ya kidemokrasia ambapo viongozi huchaguliwa au kufutwa kupitia kura.

Muhtasari
  • Ruto aidha amewakumbusha wanaopinga uongozi wake kuwa wananchi ndio watoa maamuzi na hakuna haja ya mikwaruzano ya kisiasa ya sasa.
  • Rais alitoa wito kwa Wakenya kudumisha amani na kuepuka kusababisha ghasia zinazoweza kuvunja umoja wa taifa.
RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Rais William Ruto amesema yuko tayari kukabiliana na wapiga kura 2027 hata kama alivyoonya wanaojaribu kuvuruga utawala wake.

Akijibu wito wa kujiuzulu kwa mara ya kwanza, Ruto alieleza kuwa Kenya ni nchi ya kidemokrasia ambapo viongozi huchaguliwa au kufutwa kupitia kura.

“Tujue ya kwamba pale 2027 tutafanya mtihani na hawa wananchi na kila mtu atakuja na kazi yake amefanya,” he said.

Ruto aidha amewakumbusha wanaopinga uongozi wake kuwa wananchi ndio watoa maamuzi na hakuna haja ya mikwaruzano ya kisiasa ya sasa.

Alisema wanaomtaka ajiuzulu wanapaswa kushikilia farasi wao hadi 2027 ili kuamua hatima yake juu ya nguvu ya utendakazi wake.

“Hakuna haja ya kusumbua katikati. Wacha tungoje huu mtihani kila mtu afanye tuone wa kupita nani wa zamani. Mimi najipanga, hii uchaguzi tutakutana hakuna tatizo,” alisema.

Rais alitoa wito kwa Wakenya kudumisha amani na kuepuka kusababisha ghasia zinazoweza kuvunja umoja wa taifa.

“Ninataka kuwasihi Wakenya wasilete vita, fujo au chochote ambacho kinaweza kuathiri umoja wa nchi yetu. Sisi ni taifa la kidemokrasia na katika demokrasia, watu huamua kupitia uchaguzi,” alisema.

Bila kutaja majina, Ruto alizidi kutoa matamshi ya hila akiwalenga baadhi ya watu wa kigeni ambao alidai wanasababisha machafuko ya hivi majuzi nchini.

"Ninataka kuwaambia kwamba Kenya ni taifa la kidemokrasia na hatuko karibu kuondoka," alisema.

Ruto aliyasema hayo Jumatano alipofungua rasmi kituo cha umeme cha Kimuka eneo la Kajiado Magharibi.

Mkuu wa nchi wakati huo huo alitangaza mipango ya kuwajumuisha viongozi wote katika serikali yake bila kujali itikadi zao za kisiasa.