Kenya yashuka kwenye orodha ya Moody’s

Siku ya Jumatatu, Moody’s ilishukisha Kenya kutoka “B3” hadi “Caa1”.

Muhtasari

•Kenya imeshukishwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa kupungua kwa uwezo wake wa kutekeleza mpango dhabiti wa kudhibiti deni lake.

•Orodha hiyo huanzia Aaa, Aa1, Aa2, Aa3, A1, A2, A3, Baa1, Baa2, Baa3, Ba1, Ba2, Ba3, B1, B2, B3, Caa1, Caa2, Caa3, Ca, hadi C.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Shirika la Moody’s linalokadiria viwango vya hatari katika kutoa ufadhili na mikopo kwa mataifa na mashirika limeishukisha Kenya kwenye orodha hiyo, kutokana na kile linachotaja kuwa kupungua kwa uwezo wake wa kutekeleza mpango dhabiti wa kudhibiti deni lake.

Siku ya Jumatatu, Moody’s ilishukisha Kenya kutoka “B3” hadi “Caa1”.

Orodha ya shirika hilo lina viwango tofauti, kuanzia Aaa (kumaanisha kwamba taifa liko katika hali nzuri kifedha) hadi C (kumaanisha kwamba taifa limeshindwa kulipa madeni yake, na kuna uwezo mdogo sana wa kuimarika tena).

Orodha hiyo huanzia Aaa, Aa1, Aa2, Aa3, A1, A2, A3, Baa1, Baa2, Baa3, Ba1, Ba2, Ba3, B1, B2, B3, Caa1, Caa2, Caa3, Ca, hadi C.

Kwa kulinganisha, Moody’s ilipandisha Tanzania kutoka B2 hadi B1 Mnamo Aprili 2024, na kubadilisha mtazamo wake kutoka chanya (positive) hadi thabiti (stable).

Hatua hii inajiri siku chache baada ya Rais wa Kenya William Ruto kufutilia mbali muswada tata wa fedha ambao ulipania kukusanya mapato ya ziada ya $2.7b ili kupunguza pengo katika bajeti na ukopaji wa serikali.

Rais Ruto alichukua hatua hiyo kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana wa GenZ, ambao walisema muswada huo ungewaongezea mzigo wa gharama ya maisha.

Taarifa za shirika la Moody’s hutumiwa na wawekezaji na watoaji mikopo kutathmini iwapo ni salama kuwekeza katika taifa au la, kupitia utoaji wa mikopo inayohitajika na serikali.

Kwa wawekezaji, hatua hii ya Moody’s inamaanisha kwamba ni hatari zaidi kutoa mkopo kwa serikali ya Kenya.

Aidha wale ambao wataikopesha wanaweza kudai riba ya juu kwa fedha zao, na wanaweza kupendelea kuikopesha serikali kwa muda mfupi badala ya muda mrefu, kutokana na kutokuwa na uhakika wa hali ya kifedha ya serikali.