PCS Mudavadi na DP Gachagua waponea shoka la kutupwa nje Ruto akivunja baraza la mawaziri

Rais katika hotuba yake kwa taifa, alitangaza kwamba baada ya kutathmini kwa muda mrefu, alilazimika kufanya maamuzi hao magumu ya kuwafukuza mawaziri wote kisha kuanza safari mpya ya matumaini katika serikali yake.

Muhtasari

• Hata hivyo, waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi na naibu rais Rigathi Gachagua waliponea shoka hilo kwani nyadhifa zao hazikuathirika na mageuzi hayo ya rais Ruto.

MUDAVADI NA GACHAGUA
MUDAVADI NA GACHAGUA
Image: HISANI

Rais William Ruto Alhamisi alasiri alifanya mageuzi makubwa katika baraza lake la mawaziri baada ya kulivunjilia mbali na kuwatuma mawaziri wote nyumbani.

Rais katika hotuba yake kwa taifa, alitangaza kwamba baada ya kutathmini kwa muda mrefu, alilazimika kufanya maamuzi hao magumu ya kuwafukuza mawaziri wote kisha kuanza safari mpya ya matumaini katika serikali yake.

Kando na mawaziri wote kwenda nyumbani mara moja, pia mwanasheria mkuu wa serikali, Justine Muturi alipatwa na shoka hilo.

Hata hivyo, waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi na naibu rais Rigathi Gachagua waliponea shoka hilo kwani nyadhifa zao hazikuathirika na mageuzi hayo ya rais Ruto.

“Nimeamua kuwafuta kazi mara moja Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Kenya isipokuwa Waziri mwenye mamlaka makuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora na bila shaka Ofisi ya Naibu Rais haiathiriwi kwa njia yoyote," alisema.

Ruto alisema kuwa atashiriki katika mashauriano ya kina katika sekta mbalimbali na mirengo ya kisiasa na Wakenya wengine kwa jumla.