Rais Ruto amuomboleza jaji wa mahakama ya kuu David Majanja

Jaji Majanja alifariki Jumatano jioni baada ya kifo chake kutangazwa na jaji mkuu Martha Koome

Muhtasari

•Rais alituma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Jaji Majanja,marafiki na mahakama kwa pamoja.

•Naibu rais,Gachagua pia alimtaja Majanja kama mtu aliyekuwa na taaluma ya hali ya juu katika idara ya mahakama.

Rais William Ruto
Image: screengrab

Rais William Ruto amemuomboleza jaji wa mahakama kuu David Majanja kama wakili mweledi wa uadilifu.

Jaji Majanja aliaga dunia katika hospitali ya Nairobi alipokuwa akipokea matibabu baada ya upasuaji Jumatano jioni.

Kupitia ukurasa wake wa  X, Ruto alisema Majanja alikuwa wakili mahiri ambaye uadilifu na uwezo wake vilichochea udugu wa mahakama.

“Mhe. Majanja alikuwa mwanasheria mahiri, uadilifu na uwezo wake ulichochea imani ya wafanyakazi wenzake, huku akili yake yenye nguvu ilimfanya kuwa sauti ya kutegemewa katika mahakama,” Rais Ruto aliandika.

Aidha,Rais alituma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Jaji Majanja, marafiki na mahakama, na kuongeza:

"Mwenyezi Mungu awape nguvu za kustahimili msiba huu, na roho yake ipumzike kwa amani ya milele."

Kifo cha Jaji Majanja kilitangazwa na Jaji mkuu Martha Koome, ambaye alimtaja "mtu mkuu katika maendeleo ya sheria yetu ya mabadiliko ya baada ya 2010 na nguzo muhimu" ya tume ya huduma ya mahakama (JSC) na pia idara ya mahakama kwa ujumla.

Naibu rais, Rigathi Gachagua pia alielezea masikitiko yake baada ya kufariki kwa jaji Majanja. Alisema jaji wa mahakama kuu alikuwa na taaluma ya hali ya juu katika idara ya Mahakama.

" Majanja alikuwa na kipawa cha hali ya juu ambacho kilichangia pakubwa kufafanua upya taaluma ya sheria na mfumo wa haki wa nchi yetu kwa njia mbalimbali,"  Gachagua alisema.

Majanja aliteuliwa kuwa jaji wa mahakama kuu mwaka wa 2011 na amehudumu katika maeneo ya Homa Bay, Migori, Kisumu na Kisii.