Rais William Ruto ameagiza mamlaka husika kuharakisha uchunguzi kuhusu maiti zilizokuwa zimefungwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa jalalani katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi.
Ruto amehakikishia umma kuwa waliohusika na kitendo hicho watakamatwa na kushtakiwa.
Alisema kuwa miili iliyopatikana ni tisa, ingawa wakazi wa Mukuru kwa Njenga wanasema idadi hiyo ni kubwa zaidi kwani miili mitano zaidi ilipatikana Jumamosi asubuhi.
“Kule Nairobi, kumepatikana mili ya Wakenya, imefika karibu tisa. Karibu wote ni wasichana na tunafanya uchunguzi. Nimeamrisha polisi na wale wote wanaohusika kwa mambo ya homicide. Nawahakikisha Wakenya, wale wote waliohusika na vifo vya Kware watachukuliwa hatua,” rais alisema.
Ripoti ya uchunguzi wa awali inaonyesha kuwa waathiriwa - wote ni wanawake, waliuawa kwa njia sawa.
Eneo hilo limefungwa huku polisi wakiendelea kutafuta miili zaidi.
Haya yanajiri siku moja baada ya mkuu wa polisi nchini Kenya kujiuzulu kufuatia maandamano ya kupinga nyongeza ya kodi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 40.