Tume ya kitaifa ya huduma kwa polisi (NPSC) imeorodhesha wagombeaji wa nyadhifa za naibu Inspekta Jenerali wa polisi (DIG-KPS) na naibu Inspekta Jenerali wa polisi wa utawala (DIG-APS).
Afisa mkuu mtendaji wa NPSC Peter Leley alisema walioteuliwa kuwania nafasi ya DIG-KPS ni George Adero Sedah, Eliud Kipkoech Lagat, Tom Mboya Odero na Dkt Vincent Kinas Makokha.
Wakati huo huo, tume iliwaorodhesha Gilbert Masengeli, Margaret Nyambura Karanja, James Mukuha Kamau na Dkt Masoud Mwinyi kwa wadhifa wa DIG-APS.
Wagombea hao walioteuliwa watahojiwa Jumatatu, Julai 22, 2024.Mahojiano yatafanyika katika shule ya serikali ya Kenya, chuo cha Lowe Kabete jijini Nairobi. Jumla ya watu 38 waliomba nyadhifa za naibu inspekta Jenerali huduma ya polisi ya Kenya na naibu inspekta Jenerali, huduma ya polisi ya Utawala kufuatia tangazo la tume.
Hii inafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome mnamo Julai 12. Rais William Ruto alithibitisha kujiuzulu kwa Koome na kisha kumteua DIG KPS Douglas Kanja kama kaimu IG wa NPS.
Wakati huo huo, wananchi wamehimizwa kuwasilisha taarifa zozote zinazowahusu wagombeaji kwa njia ya maandishi kwa mwenyekiti wa tume au mtandaoni mnamo au kabla ya Jumatatu wiki ijayo.