logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Blinken amtaka Rais Ruto kuzingatia maoni ya vijana kwa manufaa ya nchi

Alisisitiza umuhimu wa vijana kutumia haki yao ya kujieleza na kuandamana kama ilivyoainishwa katika sheria.

image
na Samuel Maina

Habari26 July 2024 - 08:40

Muhtasari


  • •Alisisitiza umuhimu wa uhuru wa mkutano na kujieleza kama ilivyoainishwa katika katiba ya Kenya
  • •Mjadala wao pia ulijumuisha msaada wa usalama wa kimataifa kwa Haiti ambapo Katibu Blinken alirejea msaada wa serikali ya Marekani katika operesheni za Kenya.

Waziri wa Maswala ya Nje wa Marekani Antony Blinken amemhimiza Rais William Ruto kuheshimu mchango wa vijana wa Kenya katika maendeleo ya nchi.

Kulingana na taarifa ya mazungumzo ya simu kati ya viongozi hao mnamo Alhamisi, Blinken alisisitiza umuhimu wa vijana kutumia haki yao ya kujieleza na kuandamana kama ilivyoainishwa katika sheria.

“Katibu alisisitiza umuhimu wa uhuru wa mkutano na kujieleza kama ilivyoainishwa katika katiba ya Kenya, alisisitiza jukumu muhimu linalochezwa na vijana na mashirika ya kiraia katika demokrasia bora, na alihimiza kuheshimu michango yao katika maendeleo ya Kenya,” ilisema taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Katibu Blinken pia alimuhimiza Rais Ruto kwa maagizo yake kwa Tume Huru ya Uchunguzi wa Malalamiko ya Polisi (IPOA) kuchunguza na kuwafungulia mashtaka maafisa wa polisi waliotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita.

“Katibu alimhakikishia Rais Ruto pongezi kwa ahadi yake ya uwajibikaji kwa vikosi vya usalama vilivyohusishwa na ghasia za maandamano na ahadi yake ya kuwaelekeza polisi waepuke kutumia ghasia yoyote dhidi ya waandamanaji,” taarifa ilisema sehemu yake.

Mjadala wao pia ulijumuisha msaada wa usalama wa kimataifa kwa Haiti ambapo Katibu Blinken alirejea msaada wa serikali ya Marekani katika operesheni za Kenya.

“Katibu alimshukuru Rais Ruto kwa michango ya Kenya katika operesheni ya usalama wa kimataifa nchini Haiti. Katibu alisisitiza kwamba Marekani inasimama na watu wa Kenya wanapojitahidi kujenga Kenya yenye umoja na ustawi,” taarifa iliongeza.

Kwa sasa, Kenya imetuma zaidi ya maafisa wa polisi 600 kwenda Haiti ili kushughulikia ghasia zinazotokana na magenge yaliyoathiri taifa hilo kwa miaka mingi. Marekani iliahidi kutoa zaidi ya shilingi  bilioni 39 kusaidia ujumbe huo.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yanakuja huku Wakenya wakitaka haki kwa waandamanaji waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), katika ripoti yake ya hivi karibuni, inasema kuwa idadi ya waliokufa katika maandamano imefikia 60 huku walioelezwa kupotea wakiwa 66.

Tume ya haki za binadamu imehimiza serikali kuachilia wale waliotekwa nyara na kutoa fidia kwa familia zilizothirika.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved