Hassan Joho: “Nilipata D- kwenye KCSE lakini sasa nina digrii 2 na niko mbioni kupata PhD”

Alisema kwamba suala kuhusu elimu yake liliibuliwa 2007 wakati alikuwa anawania ubunge, akiambiwa kwamba hata cheti chake cha chekechekea kilikuwa feki.

Muhtasari

• Joho alisema kwamba imekuwa kawaida kuulizwa maswali kuhusu elimu yake kwani si jambo geni kwake kila mara anapopata nafasi ya kujitetea mbele ya watu.

ALI HASSAN JOHO.
ALI HASSAN JOHO.
Image: FACEBOOK

Aliyekuwa gavana wa Mombasa ambaye sasa jina lake limependekezwa na rais Ruto kama waziri wa madini ya uchumi wa baharini, Ali Hassan Joho ameelezea kuhusu elimu yake na utajrii wake.

Akijitetea mbele ya jopo la wabunge wanaowapiga msasa mawaziri wateule, Joho alisema kwamba licha ya kupata alama ya D- kwenye mtihani wa kidato cha nne, aliweza kujisatiti na kubadilisha matokeo hayo na sasa ana shahada mbili.

Joho alisema kwamba alipata kutiwa moyo katika safari ya masomo na msomi profesa Ali Mazrui, akisema kwamba wengi wa Wakenya huwa wanawatilia shaka Wapwani katika suala la kuweza kujieleza vizuri katika lugha ya Kiingereza.

“Mimi nilipata kutiwa moyo kutoka kwa Profesa Ali Mazrui. Mazrui hakufaulu katika mtihani wake ili kupata digrii yake. Mimi nataka Wakenya wajue kwamba mihangaiko ya kihistoria ni kitu cha kweli.”

“Bwana Spika kama utangalia katika CV yangu, ilinilazimu kuchukua likizo ya mwaka mmoja nikimaliza elimu ya msingi kuenda ile ya upili. Ni kwa sababu wazazi wangu hawangeweza kunilipia karo ya shule,” alisema.

“Kilichonipa motisha ni kwamba tuliweza kubadilisha. Wakati nilipata fursa kidogo ya kujiendeleza kibinafsi, niliikwapua… ni kweli sikufanya vizuri katika mtihani wangu wa KCSE, bila kuficha nilipata D- lakini niliweza kubadilisha matokeo hayo, leo hii vile nimeketi hapa ninamiliki digrii mbili na niko mbioni kupata Phd yangu kutoka kwa chuo cha kifahari duniani,” Joho alisema.

Joho alisema kwamba imekuwa kawaida kuulizwa maswali kuhusu elimu yake kwani si jambo geni kwake kila mara anapopata nafasi ya kujitetea mbele ya watu.

Alisema kwamba suala kuhusu elimu yake liliibuliwa 2007 wakati alikuwa anawania ubunge, akiambiwa kwamba hata cheti chake cha chekechekea kilikuwa feki.