• KeNHA Jumanne ilitangaza kuwa huenda Wakenya wakaanza kulipia ada ya ushuru ikiwa Sera ya Ushuru wa Barabara ambayo kwa sasa iko kwenye kiwango cha majadiliano itaidhinishwa.
Katibu mkuu wa chama cha ODM ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna ameikashifu Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) kuhusu pendekezo lake la kutaka baadhi ya barabara kuu humu nchini kuanza kulipiwa ada za ushuru.
Akitumia jukwaa lake la X (zamani la Twitter) siku ya Jumanne, Sifuna alishangaa jinsi Mamlaka itakavyobuni sera za kutoza ushuru katika barabara zinazojengwa kwa ushuru wa Wakenya.
Aliapa kushinikiza kuitishwa kwa maafisa wa KeNHA kwenye Seneti ili waweze kufafanua sera hizo mpya.
“Sijui jinsi gani @KeNHAKenya inahalalisha pendekezo la kuanza kutoza barabara zilizojengwa na pesa za walipa kodi miaka iliyopita. Jenga barabara mpya za ushuru mchukue pesa lakini huwezi kuanza kututoza kwa kutumia barabara ya Thika bwana! Wacha tumalize na Kawira niwaite pale Senate mjieleze,” Alisema.
KeNHA Jumanne ilitangaza kuwa huenda Wakenya wakaanza kulipia ada ya ushuru ikiwa Sera ya Ushuru wa Barabara ambayo kwa sasa iko kwenye kiwango cha majadiliano itaidhinishwa.
Baadhi ya barabara zinazopendekezwa kuzingatiwa ni pamoja na Thika Superhighway, Nairobi Southern Bypass, Nairobi-Nakuru-Mau Summit Highway, Kenol-Sagana-Marua Road, Mombasa Southern Bypass na njia mpya iliyofunguliwa ya Dongo Kundu.