Katibu katika wizara ya elimu, Idara elimu ya juu na utafiti Beatrice Inyangala ametoa ufafanuzi kuhusu viwango mbalimbali vya karo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kuanzia mwezi ujao.
Kupitia jukwaa lake la X, Inyangala alifafanua kwa wepesi akisema kwamba mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya chuo kikuu utakuwa unazingatia zaidi uwezo wa wazazi kwa kuangalia mapato ya kila familia ambayo mwanafunzi anayejiunga na chuo kikuu ametoka.
Inyangala alieleza kwamba wanafunzi hao watagawanywa kwa makundi matano kulingana na uwezo wa familia zao.
Kundi la kwanza litakuwa la wanafunzi wanaotoka katika familia zenye mapato yasiyozidi Sh5,995 kwa mwezi, kundi la pili wakiwa wale kutoka kwa familia zenye mapato yasiyozidi Sh23,670 kwa mwezi.
Kundi a tatu ni wanafunzi wanaotoka familia zenye kipato kisichozidi Sh70,000 kwa mwezi, kundi la nne wakiwa wale wanaotoka familia za kipato kisichozidi Sh120,000 na kundi la 5 likiwa wanafunzi kutoka familia zenye kipato zaidi ya Sh120,000 kwa mwezi.
Kwa wanafunzi wanaotoka familia zenye kipato chini ya Sh5,995 kwa mwezi, serikali itafadhili hadi 70% ya karo yao huku mkopo wa HELB ukiwalipia 25% ya karo hivyo kuiachia familia kusimamia 5% iliyosalia.
“Kundi la 2, ufadhili wa serikali utafikia 60%, mkopo utafikia 30%, na kufanya jumla ya msaada 90%. Familia itachangia 10%, na mkopo wa uhifadhi utakuwa Sh55,000,” Inyangala alieleza.
Kwa kundi la 3, ufadhili wa serikali utafikia 50%, mkopo utafikia 30%, na kufanya jumla ya msaada 80%. Familia itachangia 20%, na mkopo wa uhifadhi utakuwa Sh50,000.
PS Inyangala alieleza pia kwamba kundi la nne, ufadhili wa serikali utafikia 40%, mkopo utafikia 30%, na kufanya jumla ya msaada 70%. Familia itachangia 30%, huku kundi la 5 likisalia bila ufadhili kutokana na dhana kwamba ni wenye navyo.