“Usiniamuru na usinishike!” Wanjigi amwambia afisa wa polisi baada ya kujiwasilisha kuhojiwa

“Usiniamuru, usinishike, unanielewa? Kuwa na heshima, usinipe masharti, kaa kimya,” Wanjigi alimuambia afisa huyo wa polisi.

Muhtasari

• Polisi wanadai walipata vitoa machozi miongoni mwa vitu vingine kwenye lango lake huko Muthaiga, Nairobi siku ya maandamano ya Nane Nane.

JIMMY WANJIGI KATIKA KITUO CHA POLISI CHA NAIROBI AREA.
JIMMY WANJIGI KATIKA KITUO CHA POLISI CHA NAIROBI AREA.
Image: HISANI

Mfanyibiashara Jimmy Wanjigi amewasili alasiri la leo katika makao makuu ya DCI kwa mwaliko wa kufanyiwa usaili kuhusu madai ya kufadhili maandamano ya Gen Z ya Agosti 8.

Baada ya kuwasili katika kituo cha polisi cha Nairobi Area akiwa ndani ya gari lake la Mercedes Benz lenye namba binafsi za usajili, Wanjigi alishuka na kumkabili afisa wa polisi aliyemtaka kutozungumza na makumi ya wanahabari waliofika langoni.

Wanjigi aliyeonekana mkali kwa polisi huyo alimnyamazisha akimtaka kutomuamuru na baadae akaingia ndani ya gari.

“Usiniamuru, usinishike, unanielewa? Kuwa na heshima, usinipe masharti, kaa kimya,” Wanjigi alimuambia afisa huyo wa polisi ambaye alijitetea akimwambia kuwa sio kumuamuru.

Polisi wanadai walipata vitoa machozi miongoni mwa vitu vingine kwenye lango lake huko Muthaiga, Nairobi siku ya maandamano ya Nane Nane.

Hii ni baada ya Agosti 8 kujaribu kumkamata nyumbani kwake bila mafanikio. Kikosi cha polisi kilivamia nyumba yake wakimtafuta.

Baadaye Wanjigi alielekea kortini ambapo alipata amri ya kuzuia kukamatwa kwake. Mahakama mnamo Agosti 16 iliongeza muda wa maagizo ya kuwazuia polisi kumkamata.

Jaji Bahati Mwamuye aliongeza agizo hilo hadi Septemba 19 lakini wakati huo huo alisema hangeweza kutoa amri ya kukomesha usajili wa karatasi ya mashtaka dhidi ya Wanjigi.

Jaji alisema ombi lililowasilishwa na Wanjigi liligusia tu masuala ya kukamatwa na wala si kufunguliwa mashtaka.