Waliokamatwa wakikojoa na kutupa taka Nairobi wapewa adhabu ya kufanya usafi City Mortuary

Afisa Mkuu wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria alikaribisha ‘adhabu’ ya huduma ya jamii, na kuthibitisha kuwa itakuwa fundisho kwa wale wanaonuia kuendelea kuvunja sheria.

Muhtasari

• Afisa Mkuu wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria alikaribisha ‘adhabu’ ya huduma ya jamii, na kuthibitisha kuwa itakuwa fundisho kwa wale wanaonuia kuendelea kuvunja sheria.

CITY MORTUARY
CITY MORTUARY
Image: HISANI

Watu zaidi ya 30 waliokamatwa Jumatatu usiku kwa kukojoa na kutupa uchafu katika mitaa ya Nairobi sasa watatumikia vifungo vya huduma za jamii katika vituo vya umma ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika makafani ya Nairobi Funeral Home, awali ikiitwa makafani ya City.

Mahakama ya jiji ilitoa hukumu hizo siku ya Jumanne kufuatia kufikishwa mahakamani kwa watu waliokamatwa katika msako mkali wa maafisa wa idara ya mazingira ya kaunti ya Nairobi.

Mahakama iliwapa wahalifu wengine kufagia mitaa iliyochaguliwa katikati mwa jiji huku wengine wakisafisha bustani ya Uhuru ambayo imesalia kufungwa kwa umma tangu matukio makubwa ya Juni 25 wakati waandamanaji wanaoipinga serikali walipoharibu kituo hicho.

Akihutubia wanahabari katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City, Afisa Mkuu wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria alikaribisha ‘adhabu’ ya huduma ya jamii, na kuthibitisha kuwa itakuwa fundisho kwa wale wanaonuia kuendelea kuvunja sheria.

“Nairobi yetu ya leo sivyo ilivyokuwa hapo awali, na kwa sasa, kila mtu anapaswa kutunza mazingira. Ni makosa sana kwa watu kukojoa na kutupa takataka mahali popote ndani ya CBD,” alisema.

Mosiria aliwataka wakaazi wa jiji kujifahamu na sheria ndogo za jiji na Sheria ya Kero ya Umma ya Nairobi ya 2021.

"Kama kaunti, tutahakikisha kwamba sheria ndogo za jiji letu [zinafuatwa]," Mosiria alisema.

Aliwaonya wengine kuvunja sheria za kaunti za vikwazo sawa.

Kulingana na Sheria ya Kero ya Umma ya Nairobi 2021, kukojoa au kujisaidia haja kubwa katika eneo la umma kunatozwa faini ya Sh10,000, kifungo cha miezi sita jela au zote mbili.