Mzozo wa kutatanisha ulishuhudiwa katika jiji la Nairobi katika barabara ya River Road,baina ya wahudumu wa matatu na polisi wa trafiki,jambo ambalo lilizua mfarakano baina yao na kusababisha hali ya sitofahamu.Chanzo cha mzozo huo hakijabainika kufikia sasa.
Wakati hali hiyo inashuhudiwa,manamba mmoja alimpiga konde askari mmoja wa trafiki na kumjeruhi kichwani.Kutokana kisa hicho iliwabidi maafisa wa kudumisha amani kuingilia kati ili kutenganisha pande zote mbili ambazo zilikuwa zimejawa na ghadhabu si haba.
Aidha,mhusika mkuu wa kitendo hicho alionekana kukataa kutiwa mbaroni jambo ambalo liliongeza kero kwa maafisa hao wa usalama.
Hata hivyo,Wakenya wamekashifu vikali kitendo cha askari mmoja ambaye alionekana kuchomoa bunduki lake tayari kufyatua lakini akazuiliwa kwenye kisanga hicho na wakaazi waliojitokeza kushuhudia kisanga hicho kisicho na utulivu.
Kwenye picha ambazo zimesambaa mitandaoni mjeruhiwa anaonekana ameshika kichwa chake kwa maumivu huku raia wakimwelekeza kuaga eneo la tukio.Damu ilisambaa katika eneo hilo ni idhibati tosha kuwa askari huyo alipata majeraha.
Vinginevyo ni jambo ambalo limezua taharuki baada ya polisi mdumisha amani kutaka kufyatua risasi,wengi wakilalama mitandaoni,'kila polisi lazima aheshumu mamlaka yao,hili ni suala la trafiki badala ya AP.Kwanini uko tayari kutumia bunduki katika kesi kama hiyo' Mmoja alisema.