• Kebaso alitangaza kuwa ataanza ziara yake Kenya mzima kuitatmini hali ya miradi iliyozinduliwa na rais Ruto.
• Alisema lengo la ziara zake ni kuweka ukweli wazi na kuwapa wananchi elimu ya kiraia kama njia moja ya kuwatayarisha kufanya maamuzi bora wakati wa uchaguzi.
Morara Kebaso, jamaa anayezunguka Kenya yote kutumbua miradi hewa ya serikali na kuwapa Wapiga kura elimu ya kiraia amefichua kupokea gari ambalo atakuwa analitumia katika ziara zake.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso alichapisha picha za gari hilo la kifahari, siku chache baada ya kuomba wahisani kumpa mchango wa kununua mitambo ya kutumia wakati wa ziara zake katika maeneo ya miradi mbalimbali inayozinduliwa na rais Ruto.
“Wabunifu wa Picha. Ni wakati wanu wa kufanya Kazi ya Bwana. Gari ya kuweka public address system tumepata. Tunahitaji muundo wa kuweka chapa na kufunga Cheza kama nyinyi haraka haraka kwa maoni ama DM,” Kebaso alisema.
Kebaso alitangaza kuwa ataanza ziara yake Kenya mzima kuitatmini hali ya miradi iliyozinduliwa na rais Ruto, akisema kwamba ataanzia kaunti za uliokuwa mkoa wa Kati kuanzia Ijumaa Septemba 6.
“Msafara wa Kuzindua upya, Mlima Kenya Utaanza Ijumaa tarehe 6. Murang’a, Kirinyaga, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Isiolo. Meet Up Point ni Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Old Kenyatta karibu na Unicity Mall. Kama kawaida hakikisha umeweka bajeti ya mafuta/nauli, chakula na matunzo. Zingatia hii ni kampeni dhidi ya Utawala Mbovu na Ufisadi,” alisema.
Wakili huyo ambaye pia ni mfanyibiashara wa fenicha alisema lengo la ziara zake ni kuweka ukweli wazi na kuwapa wananchi elimu ya kiraia kama njia moja ya kuwatayarisha kufanya maamuzi bora wakati wa uchaguzi.
“Dhamira ni kufanya ukweli ujulikane na kushirikisha umma kuhusu jinsi tunavyoweza kufanya maamuzi bora kwenye kura. Pia tutazungumza kuhusu ukaguzi wa kiraia na uwajibikaji. Walinunua upinzani na kuweka bungeni mfukoni. Walifikiri hatuna uwezo na tunaogopa kutekwa nyara na kuteswa. Tutaandika upya hadithi yetu,” aliongeza.
Wakati uo huo, baadhi ya watumizi wa mtandao wa X wameunda mabango madogo wakimpigia debe Morara Kebaso kushirikiana na mkwasi Jimmy Wanjigi kuwania urais, yeye akiwa kama mgombea mwenza wa Wanjigi.