•Uchambuzi huo wa hivi karibuni zaidi ulijumuisha tafiti 63 kutoka 1994-2022, zilizochambuliwa na wachambuzi 11 kutoka nchi 10.
•"Hakuna jambo kati ya mambo makuu yaliyochambuliwa lililoonyesha hatari ya kupata saratani," anasema.
Hakuna uhusiano kati ya matumizi ya simu ya mkononi na kuongezeka hatari ya kupata saratani ya ubongo, kulingana na uchambuzi mpya uliofanywa kwa ajili ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kwa kukusanya ushahidi wa tafiti zilizochapishwa ulimwenguni.
Licha ya ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia ya simu, hakujawa na ongezeko la matukio ya saratani ya ubongo, uchambuzi huo uliochapishwa Jumanne umegundua. Hilo ni hata kwa watu wanaopiga simu kwa muda mrefu au wale ambao wametumia simu kwa zaidi ya miaka kumi.
Uchambuzi huo wa hivi karibuni zaidi ulijumuisha tafiti 63 kutoka 1994-2022, zilizochambuliwa na wachambuzi 11 kutoka nchi 10, pamoja na mamlaka ya ulinzi dhidi ya mionzi ya serikali ya Australia.
"Uchambuzi huo ulitathmini athari za masafa ya redio, yanayotumiwa katika simu na vile vile TV, kamera za kufuatilia watoto na rada," anasema mhusika katika uchambuzi huo na profesa wa magonjwa ya saratani katika Chuo Kikuu cha Auckland, New Zealand, Mark Elwood.
"Hakuna jambo kati ya mambo makuu yaliyochambuliwa lililoonyesha hatari ya kupata saratani," anasema.
Mapitio hayo yaliangalia saratani za ubongo kwa watu wazima na watoto, na vile vile saratani ya tezi ya kuzalisha homoni katika ubongo, tezi za mate na saratani ya damu, na hatari zinazohusiana na matumizi ya simu, minara ya simu, vifaa vya kusambaza mawasiliano, pamoja na vifaa vingine vinavyohusiana na simu.
Aina zingine za saratani zitaripotiwa katika uchambuzi tofauti.
WHO na mashirika mengine ya afya ya kimataifa yamesema hapo awali hakuna ushahidi wa uhakika wa madhara ya kiafya kutokana na mionzi ya simu za mkononi, lakini ilitaka utafiti zaidi.
Kundi la ushauri la WHO limetaka uchambuzi huo kuchapishwa upya haraka iwezekanavyo kutokana na taarifa mpya tangu tathmini yake ya mwisho mwaka 2011. Tathmini hiyo ya WHO itatolewa katika robo ya kwanza ya mwaka ujao