Serikali imedumisha marufuku ya shughuli za kijamii shuleni ikiwa ni pamoja na siku za maombi, kutembelea shule wakati wa muhula wa tatu.
Katibu Mkuu wa Elimu Belio Kipsang aliamuru utekelezwaji mkali wa marufuku hiyo na shule zote nchini, wiki moja baada ya wanafunzi kurejea shuleni kwa muhula wa tatu.
“Madhumuni ya waraka huu ni kuwataka mtekeleze agizo hilo kwa kuhakikisha shule hazifanyi shughuli zozote kati ya hizo. Tafadhali leta yaliyomo katika waraka huu kwa shule zote zilizo chini ya mamlaka yako,” alisema Kipsang katika barua hiyo aliyowaandikia wakuu wa elimu katika kaunti zote nchini.
Serikali kupitia wizara ya elimu ilitangaza msimamo wake kuhusu watu wa nje kuruhusiwa kufanya ziara shuleni muhula wa tatu mnamo Januari 2021, wakati mareemu George Magoha alikuwa waziri.
Hata hivyto, mara ya kwanza kwa marufuku ya aina hiyo kutangazwa shuleni ilikuwa 2016 wakati aliyekuwa waziri Fred Matinag’i alitangaza kusitishwa kwa shughuli zozote zisizohusiana na masomo shuleni wakati wa muhula wa tatu.
Kwa kawaida, muhula wa tatu huwa mfupi na wakati uo huo ndio wanafunzi wanajiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Matiang’i akitangaza marufuku hiyo, alisema ilikuwa ya maana kwani watu wengi walikuwa wanaruhusiwa kutangamana na watahiniwa na kuwahadaa kuhusu uwezekano wa kudanganya katika mitihani ya kitaifa.
Ili kuzuia usumbufu huu wa kifikira kwa watahiniwa, waziri huyo wa zamani alipiga marufuku watu wasio walimu kuruhusiwa kuingia shuleni muhula wa tatu.