Nimempoteza mlezi, babake Cheptegei asema kuhusu kifo cha mwanae

"Nimepoteza binti ambaye amekuwa akisaidia kwa njia nyingi," alisema.

Muhtasari

•Babake marehemu Rebecca Cheptegei ameelezea masikitiko makubwa kwa kumpoteza binti yake huku akitaka haki itendeke.

•Cheptegei aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret.

Image: BBC

Mzee Joseph Cheptegei, babake marehemu mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei ameelezea masikitiko makubwa kwa kumpoteza binti yake huku akitaka haki itendeke.

Cheptegei ambaye alikuwa akihutubia wanahabari katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret muda mfupi baada ya kupokea habari hizo alisema kuwa familia hiyo sio tu imempoteza binti mpendwa bali pia mlezi.

"Nimepoteza binti ambaye amekuwa akisaidia kwa njia nyingi," alisema.

Akitaja kifo hicho kuwa kichungu kwake, Cheptegei aliyeonekana kufadhaika alisema kama familia wamekuwa wakimtegemea, haswa katika kusaidia elimu ya wadogo zake.

"Tuna watoto katika shule za sekondari na sijui ni jinsi gani tutakabiliana na changamoto hii ili kuhakikisha wanamaliza masomo yao," aliongeza.

Pia alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kuharakisha uchunguzi na kuhakikisha mhalifu wa kitendo hicho cha kinyama anakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Ni lazima tukabiliane na ukatili wa kijinsia! Waziri wa michezo Kenya

Wakati huo huo, waziri wa michezo nchini Kenya, Kipchumba Murkomen amemuomboleza mshikilizi wa Rekodi ya Wanawake Marathon Rebecca Cheptegei, akisema kifo chake ni hasara kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Murkomen katika taarifa aliotoa siku ya Alhamisi alisema kifo chake ni ukumbusho kwamba juhudi zaidi zinafaa kuwekwa ili kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

Marehemu Cheptegei anasemekana alipata asilimia 80 ya majeraha ya moto baada ya anayedaiwa kuwa mpenzi wake kumwagia mafuta ya petroli mwilini mwake na kumchoma moto.

Kuchomoka huko kuliharibu viungo vyake vingi vya mwili.

Cheptegei aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret.

Aliendelea kusema kuwa serikali ya Kenya imejitolea haki inatendeka kwa Rebecca.

Cheptegei alikuwa na umri wa miaka 33 na amekuwa mwanariadha kwa zaidi ya miaka 15.