KQ yavunja kimya baada ya shughuli kuvurugwa JKIA kutokana na mgomo wa wafanyikazi

Wafanyikazi katika uwanja wa JKIA waliweka zana zao chini mwendo wa saa sita usiku wa Jumanne.

Muhtasari

•KQ imetoa taarifa ikiwahutubia wateja wake kuhusu kutatizwa kwa huduma katika Uwanja wa JKIA usiku wa kuamkia Jumatano.

•KQ imesema wanaangalia hali ilivyo katika uwanja huo na kuahidi kutoa sasisho kuhusu safari za ndege zilizoathiriwa.

huku wafanyakazi wakigoma mnamo Septemba 11, 2024.
Abiria wakiwa wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku wafanyakazi wakigoma mnamo Septemba 11, 2024.
Image: FELIX KIPKEMOI

Kampuni ya Usafir wa Ndege ya Kenya Airways (KQ) imetoa taarifa ikiwahutubia wateja wake kuhusu kutatizwa kwa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta usiku wa kuamkia Jumatano.

Wafanyikazi katika uwanja wa JKIA waliweka zana zao chini mwendo wa saa sita usiku wa Jumanne huku wakipinga pendekezo la uchukuaji uliopendekezwa wa uwanja huo mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na shirika la India la Adani Group.

Katika taarifa yake Jumatano asubuhi, shirika la ndege la Kenya Airways lilitangaza kuwa mgomo wa wafanyikazi ulisababisha kucheleweshwa na kughairiwa kwa baadhi ya safari za ndege.

"Kenya Airways ingependa kukuarifu kwamba kutokana na hatua ya baadhi ya wafanyakazi wa JKIA, hii imesababisha baadhi ya ucheleweshaji na uwezekano wa kughairiwa kwa baadhi ya safari zetu kwa abiria wanaoondoka na wanaowasili," KQ ilisema katika taarifa.

Kampuni hiyo ilibaini kuwa wanaangalia hali ilivyo katika uwanja huo wa ndege na kuahidi kutoa sasisho kuhusu safari za ndege zilizoathiriwa.

"Asante kwa kuelewa na ushirikiano," kampuni hiyo ilisema.

Misururu mirefu ilishuhudiwa Jumanne usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku wafanyikazi wa anga wakianza mgomo.

Mgomo huo unafuatia notisi iliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga (KAWU) mnamo Agosti 12, 2024, ambapo walipinga pendekezo la kukodisha uwanja wa ndge wa kimataifa JKIA kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema, akitoka notisi ya mgomo, alisema kuwa mkataba wa JKIA-Adani ungesababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi wengi, kuajiriwa kwa wafanyikazi wa kigeni, pamoja na mazingira duni ya kazi.

Wafanyakazi hao walitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) na mameneja watatu wakuu kujiuzulu, wakiwashutumu kwa uzembe na kushughulikia vibaya mpango huo.

Aidha walitaka mameneja wawili wa usalama wa shirika la ndege la Kenya Airways kujiuzulu wakitaja utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na shutuma za ulanguzi wa binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, na kupandishwa vyeo kwa njia isiyo ya haki ndani ya idara hiyo.

Mgomo huo siku ya Jumanne usiku ulisababisha ratiba za safari za ndege kuvurugika, huku abiria wengi wakikwama kwenye uwanja wa ndege.

Wafanyakazi hao wameapa kuvuruga shughuli za kawaida hadi pale serikali itakapositisha mkataba wake na Adani.