Bonface Mwangi afichua sababu ya kutaka kujiua mwezi uliopita

Mwangi alisema kwamba fikira ya kutaka kujiondoa duniani mwenyewe zilisukumwa na matukio ambayo yalikuwa yamejiri nchini kwa wakati huo – kuona umwagikaji wa damu wa vijana waliokuwa wanaandamana.

Muhtasari

• Hata hivyo, hakuweza kufanikisha fikira zake kwani familia yake ilimfika karibu na kumpa msaada mkuu wa kumtafutia matibabu na ushauri nasaha wa kiakili.

BONFACE MWANGI
BONFACE MWANGI
Image: FACEBOOK

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Bonface Mwangi amefichua kwamba mwezi mmoja uliopita, alifikiria kujitoa uhai.

Kupitia ujumbe mrefu aliouchapisha kwenye ukurasa wake w X, Mwangi ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kuongoza maandamano ya kupinga serikali ya rais Ruto alisema kwamba alijikuta katika kiza kinene ambapo chaguo pekee akilini mwake lilikuwa ni kujitoa uhai.

Mpiga picha huyo wa zamani alifichua kwamba alikuwa anamaanisha uamuzi wake huo, kiasi kwamba alikuwa tayari ameandika wosia wake na hata kuwapigia simu ya mwisho baadhi ya watu wake wa karibu.

“Mnamo Agosti 3, 2024, nilijipata mahali penye giza sana na nikafikiria kujiua. Siku chache mapema, nilikuwa nimetia saini wosia wangu, kisha nikapiga simu au kutuma ujumbe mfupi kwa watu wachache. Ilikuwa ni kuaga kwangu. Nilitaka kufa. Ondoka kwenye ulimwengu huu kwa wema,” alisema.

Mwangi alisema kwamba fikira ya kutaka kujiondoa duniani mwenyewe zilisukumwa na matukio ambayo yalikuwa yamejiri nchini kwa wakati huo – kuona umwagikaji wa damu wa vijana waliokuwa wanaandamana.

“Kulikuwa na maumivu mengi sana, huzuni, na kiwewe maishani mwangu hivi kwamba sikuweza kustahimili tena. Sikuweza kuendelea kutazama bila msaada huku nchi yetu ilipokuwa ikiingizwa katika mzozo mbaya wa ghasia zilizoidhinishwa na Serikali, zikilenga Wakenya wasio na hatia,” alifunguka.

Hata hivyo, hakuweza kufanikisha fikira zake kwani familia yake ilimfika karibu na kumpa msaada mkuu wa kumtafutia matibabu na ushauri nasaha wa kiakili.

Mwezi mmoja baada ya kutoweka katika mitandao ya kijamii, Mwangi amerejea kwa kishindo na kusema sasa yuko katika hali shwari kiakili na amepata mwamko mpya kimaisha.

“Ingawa nilitaka kujiua, familia yangu na marafiki waliniwekea pete ya upendo na huruma iliyonifanya nifikirie upya. Walinilazimisha kutafuta usaidizi wa kitaalamu, na kuchukua mapumziko ya kiafya ili kuzingatia ustawi wangu wa kiakili.”

“Hiyo ilisaidia kuniweka katikati tena. Nina maisha mapya sasa, na ninathamini sana upendo mkuu na usaidizi ambao ulitolewa kwangu na familia yangu wakati huo ambapo giza lilitishia kutushinda.” Alimaliza.