Maneno 'Kitu Kidogo' na 'Panya route' yaongezwa katika Kamusi ya Kizungu ya Oxford

'Kitu kidogo' humaanisha hongo ilhali 'panya route' linamaanisha njia ya mkato

Muhtasari

• Maneno hayo yameidhinishwa rasmi  kuwa ya Kimbombo katika kamusi ya Kiingereza ya Oxford.

• Asili ya maneno hayo ni Afrika Mashariki na yametumika sana nchini Kenya kwa muda mrefu tangu miaka ya tisini. 

Image: HISANI

Misemo maarufu ya lugha ya Kiswahili Kitu Kidogo na Panya Route sasa ni rasmi kuwa ni maneno ya lugha  ya Kiingerza baada ya kamusi ya kimombo ya Oxford kuyaidhinisha.

Meneja wa utangazaji wa vyombo vya habari vya chuo kikuu cha Oxford amesema hayo kupitia ujumbe rasmi.

Msemo 'kitu kidogo' nchini Kenya linamaanisha hela zinazotolewa kwa njia isiyo ya haki ili kufanyiwa kitu fulani. Jina hilo ni sawa na kusema hongo au rushwa.

Neno 'panya route' nalo linamaanisha njia ya mkato au njia ya siri inayotumika kusafirisha bidhaa za magendo.

Kamusi ya kizungu ya Oxford ndiyo imekubalika katika sehemu nyingi za dunia kama kamusi rasmi yenye mamlaka ya lugha ya kimombo.

Ili neno kuidhinishwa katika kamusi hiyo, ni lazima lizingatiwe kutoka kwa watumiaji mbali mbali na kuwa limetumika kwa muda mrefu.

Neno 'pesa kidogo' lilitafsiriwa katika lugha ya Kiingereza kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1993 kumaanisha 'something small' kwa sajili ya kumaanisha hongo.

Neno 'panya route' nalo ni maneno mawili ya lugha ya kiswahili na kiingereza. Panya kwa tafsiri ya Kiingereza ni 'rat' ilhali 'route' kwa kiswahili ni njia.

Maneno 'panya route' na 'kitu kidogo' ni maneno ya kiswahili ambayo yameingizwa kwa kamusi la Kiingereza yakiongeza idadi ya maneno ya Kiswahili kwa lugha ya Kiingereza.

Maneno mengine ya Kiswahili kwenye kamusi ya Oxford ni ikiwemo Mzee, Mwalimu, nyama choma, jembe, sheng, mandazi, isukuti muratina, chapati, githeri, asante sana, na jambo.