Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa yatangaza kuongezeka kwa mvua, yataja maeneo yatakayoshuhudia mvua kubwa

Wakenya wamehimizwa kujiandaa kwa ajili ya ongezeko la mvua linalotarajiwa katika maeneo mengi nchini.

Muhtasari

•Idara ya utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya ilionya kwamba kuongezeka kwa kiwango cha mvua kunatarajiwa kutoka Alhamisi hadi wikendi.

•Idara hiyo ilitaja maeneo mbalimbali ya nchi ya Kenya ambayo yanatarajiwa kushuhudia mvua kubwa katika siku zijazo.

Mvua kubwa inakuja
Image: HISANI

Wakenya wamehimizwa kujiandaa kwa ajili ya ongezeko la mvua linalotarajiwa katika maeneo mengi nchini katika siku kadhaa zijazo.

Katika taarifa ya Jumatano, Idara ya utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya ilionya kuwa kuongezeka kwa kiwango cha mvua kunatarajiwa kutoka Alhamisi hadi wikendi.

Kufuatia hali hiyo, idara hiyo imewataka wakenya kuwa waangalifu zaidi huku mvua hiyo kubwa ikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali.

"Tazamia kuongezeka kwa kiwango cha mvua katika maeneo mengi ya nchi kuanzia Alhamisi hadi wikendi. Kaa salama na mkavu, kila mtu!” Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ya Kenya ilionya.

Idara hiyo ilitaja maeneo mbalimbali ya nchi ya Kenya ambayo yanatarajiwa kushuhudia mvua kubwa katika siku zijazo.

Maeneo hayo ni pamoja na Nyanda za Juu Mashariki/Magharibi mwa Bonde la Ufa, Eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Maeneo ya Nyanda za Juu Kusini-mashariki, na maeneo ya Kaskazini-magharibi na Kaskazini-mashariki.

Siku ya Jumatano, Papa Francis ametuma ujumbe wa kuwafariji Wakenya wakati nchi  ikikabiliwa na mafuriko makubwa.

Katika ujumbe wake wa siku ya Jumatano, 1 Mei 2024, Papa alitoa wito wa kuiombea nchi ya Kenya wakati wananchi wanakabiliana na makali ya mafuriko.

Alisema kwamba yeye binafsi anawaombea Wakenya ambao wanakabiliwa na athari za mafuriko ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya takriban watu 200.

"Niko karibu kiroho na watu wa Kenya wakati huu ambapo mafuriko makubwa yamegharimu maisha ya watu wengi na kuharibu maeneo makubwa. Tuwaombee kwa pamoja wale wote wanaopatwa na maafa haya ya janga," Papa alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X.

Haya yanajiri kufuatia mafuriko yanayoendelea nchini ambayo yamesababisha uharibifu wa maisha na mali.

Jumatano asubuhi, wakaazi wa Kitengela walikumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha katika jiji hilo na viunga vyake.

Wengi wao walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuomba usaidizi huku mashirika ya kibinadamu kama vile Msalaba Mwekundu wa Kenya yakichukua hatua ya kuzihamisha familia.

Wakaazi kadhaa hawakuweza kutoka nje ya nyumba zao mapema saa mbili asubuhi Jumatano kwa sababu ya hali ya mafuriko.

Taarifa za hivi punde kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya zinaonyesha kuwa angalau watu 11, sita kati yao wakiwa katika hali mbaya, walikuwa wamehamishwa.

Siku ya Jumanne, Rais William Ruto alitangaza kuwa mafuriko hayo yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 170.